VICTORIOUS WOMEN GROUP WAFANYA MATENDO YA HURUMA KWA AKINA MAMA WAJAWAZITO KITUO CHA AFYA KATORO

Kikundi cha Victorious Women Group kimekabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa akina mama wajawazito na waliojifungua katika Kituo cha Afya Katoro, kilichopo Wilayani na Mkoa wa Geita, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kijamii za kikundi hicho.

Msaada huo umetolewa  Agosti 30, 2026, ambapo wanachama wameamua kutenga sehemu ya kile wanachokipata na kuwasaidia wanawake wanaokabiliwa na changamoto katika kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua.

Akizungumza katika kituo hicho, Mwenyekiti wa Victorious Women Group, Esta Kiuma Samwel, amesema kikundi hicho kimeundwa kwa lengo la kuwawezesha wanawake kuinuana kiuchumi na kusaidiana wakati wa changamoto.

Amesema wameamua kuanza kutoa msaada kwa akina mama na watoto kutokana na kutambua changamoto zinazohusiana na uzazi, huku akieleza kuwa hata vitu vidogo vinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa mama anayehitaji msaada.

Esta pia amesisitiza umuhimu wa wazazi kushirikiana katika malezi ya watoto, kuhakikisha wanapata elimu bora na kulelewa katika maadili mema ili kujenga kizazi chenye nidhamu na utii.

Kwa upande wake, Edina Betha Morisi, Muuguzi wa Kituo cha Afya Katoro akimwakijisha Mganga mfawidhi, amesema uongozi wa kituo hicho unashukuru kwa msaada huo, akieleza kuwa baadhi ya wanawake wanaojifungua hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu kama sabuni na pampas kwa ajili ya watoto wao.

Amesema msaada huo umehusisha pampas, sabuni za unga na kipande, pamoja na nguo za watoto ikiwemo soksi na kofia, ambazo zitawasaidia watoto kujikinga na baridi.

Edina ametoa wito kwa vikundi vingine kuiga mfano huo na kuwakumbuka wahitaji, akieleza kuwa Kituo cha Afya Katoro kinahudumia idadi kubwa ya wanawake na watoto, huku kikisaidia kujifungua watoto kati ya mia nane hadi elfu moja kwa mwezi.

Baadhi ya akina mama waliopokea msaada huo wameishukuru Victorious Women Group na kuomba iendelee kuwa na moyo wa kuwasaidia wahitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *