Wakazi wanaoishi karibu na Ziwa Victoria katika Kata ya Butundwe Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita wanakabiliwa na changamoto ya mashambulizi ya wanyama wakali aina ya viboko ambayo imekuwa ikijirudua mara kwa mara na kusababisha vifo vya baadhi ya wakazi wa eneo.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhandisi Tumaini Magesa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo amesema ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita viboko hao wameua watu watatu katika jimbo hilo hali ambayo imezua hofu kwa wananchi.
Kwa upande wa madiwani wa kata zilizopo karibu na Ziwa Victoria wameiomba serikali kuruhusu makampuni yenye leseni za uwindaji kusaidia kuondoa viboko hao ambao wamekuwa wakihatarisha maisha ya watu ili kuwapa wananchi wa kata hizo fursa ya kuishi kwa amani.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashimu Komba amekiri kupokea taarifa hizo na kusema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Geita tayari imeanza mchakato wa kudhibiti matukio hayo.