VETA, CVM KUWAJENGEA UWEZO WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kwa kushirikiana na shirika la Kiitaliano lijulikanalo kama CVM imeanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wafanyakazi wa majumbani wenye lengo la kuwapatia ujuzi, kuwafanya waboreshe utendaji kazi wao, waheshimike, wapate haki zao na kuthaminiwa utu wao.

Hatua hiyo, imebainisha leo Februari 16,2026 Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Athony Kasore wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu jitihada za uendelezaji ufundi stadi nchna fursa kwa vijana ambapo amesema jumla ya wasichana 1,244 wamejengewa uwezo na kuwawezesha kufanya kazi za majumbani ndani na nje ya nchi.

“Mradi huu unatekelezwa kupitia vyuo vya VETA Dar es Salaam, Lindi, Tanga, Dodoma, Mikumi na Iringa. Kupitia ushirikiano huu VETA imewajengea uwezo wasichana 1,244 ili kuwawezesha kufanya kazi za majumbani ndani na nje ya nchi,”amesema. 

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo mitaala ya Mafunzo kwa Wafanyakazi Majumbani imeandaliwa, ikiwemo inayowezesha kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa kipindi cha mwezi mmoja, miezi mitatu au miezi sita. 

“Hili ni eneo jingine la fursa kwa vijana, hasa wale wanaofanya kazi hizo hapa nchini au wenye nia ya kwenda nje ya nchi kufanya kazi za namna hiyo,” amesema.

Sanjari na hayo amebainisha kuwa katika kuwapatia vijana na wananchi wengine uhuru zaidi wa kujifunza mafunzo ya ufundi stadi popote walipo na kwa muda wao, wameanzisha mfumo (application) uitwao VSOMO ambao humwezesha mwanafunzi kujifunza maarifa yote ya ufundi stadi kwa kutumia simu ya mkononi, kufanya mtihani kwenye simu hadi mwisho wa mpango wa mafunzo ya nadharia. 

“Baada ya hapo, atapangiwa kufanya mafunzo ya vitendo kwenye chuo kimojawapo cha VETA. Hii inapunguza muda wa kukaa chuoni na inaongeza matumizi bora ya simu za mkononi na muda wa mafunzo. Vilevile, mpango huu unawapa fursa watu walio mbali na vyuo kupata mafunzo ya ufundi stadi,”amesema. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *