Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amewataka vijana kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya Wilaya hiyo kwa ubunifu na maarifa, ili kujenga maisha yao, familia zao na kuchangia maendeleo ya Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kuwa wazalishaji na si watafutaji wa ajira pekee.
Masindi ametoa kauli hiyo wakati akizindua rasmi Jukwaa la Vijana la Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kishapu Sekondari, ikiwa ni jukwaa linalolenga kuwaunganisha vijana, kuwajengea uwezo na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Katika hotuba yake, DC Masindi amewataka vijana kutumia akili zao kwa faida, kufanya maamuzi yenye tija na kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo elimu, ujasiriamali, kilimo, mifugo, biashara na sekta nyingine zinazoweza kuwa chanzo cha kipato.
“Vijana hakikisheni mnajiepusha na uchochezi, vitendo vinavyokiuka taratibu na sheria za nchi, pamoja na makundi au mienendo inayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa Taifa. Badala yake, mnapaswa kuwa wazalendo, kuheshimu sheria na kutambua wajibu wenu katika kulinda amani na mshikamano wa nchi yetu,” amesema DC Masindi.

“Vijana lazima mjue kwamba Taifa linawategemea. Mnapaswa kuwa wazalishaji, mjitengenezee kipato na muweze kusaidia familia zenu. Msisubiri kila kitu mfanyiwe; tumieni fursa mlizonazo na akili zenu kuibua shughuli zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewahimiza vijana kuifahamu nchi yao kwa kusoma na kujifunza historia yake, akieleza kuwa uelewa wa historia, utamaduni na misingi ya Taifa unawasaidia vijana kujenga uzalendo, kutambua wajibu wao na kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya nchi.
Amehimiza pia umoja na ushirikiano katika masuala ya maendeleo, akiwataka vijana kushirikiana na watu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuibua fursa, kubadilishana maarifa, kupata mitandao ya kibiashara na kutafuta masoko ya bidhaa na huduma wanazozalisha.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Athuman Mchekwa, amesema Halmashauri itaendelea kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za kiuchumi, kuwawezesha kupata taarifa sahihi, kuwajengea uwezo katika ujasiriamali na uzalishaji pamoja na kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Mchekwa amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kulitumia Jukwaa hilo kama sehemu ya kujifunza, kubadilishana mawazo, kuibua fursa na changamoto zao, huku akiwataka kuwa wabunifu, wazalishaji na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Wilaya na Taifa
Katika uzinduzi huo, vijana wamepata mafunzo mbalimbali yaliyolenga kuwaongezea uelewa na uwezo wa kutumia fursa zinazowazunguka. Mafunzo hayo yamejikita katika fursa za uchumi kwa vijana ndani ya Wilaya ya Kishapu, elimu ya uraia na ujenzi wa mshikamano wa Taifa, namna ya kuibua na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika mazingira yao, pamoja na kujadili fursa za kiuchumi kwa vijana kwa msisitizo wa uadilifu, uwajibikaji, kujitolea na uzalendo kwa Taifa.

Kwa upande wao, vijana walioshiriki uzinduzi huo wameeleza kufurahishwa na kuanzishwa kwa Jukwaa hilo, wakisema limewapa nafasi muhimu ya kupata elimu, kubadilishana mawazo na kufahamu fursa ambazo awali hawakuwa na taarifa nazo huku wakiipongeza Serikali kwa kuanzisha jukwaa hilo, wakieleza kuwa daraja muhimu kati ya vijana, Serikali na wadau mbalimbali, kwa kuwa linaweza kuwawezesha vijana kutoa mawazo yao, kueleza changamoto zao, kupata taarifa za fursa na kushiriki katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo.
Uzinduzi huo umefanyika chini ya kaulimbiu “Vijana Tuyajenge Tanzania, Ni Yetu Sote”, ikisisitiza wajibu wa vijana kuwa nguvu kazi muhimu katika ujenzi wa Taifa.Kuanzishwa kwa Jukwaa la Vijana Kishapu kunatoa fursa kwa vijana kuwa na sauti katika masuala yanayowahusu, kujenga mitandao ya fursa na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.


