Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga (Ibadakuli) kutakuwa hatua kubwa ya mageuzi katika sekta za uchumi, biashara, utalii na usafiri wa anga ndani ya mkoa na kwa taifa kwa ujumla.
RC Mboni amezungumza hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa mkoa huo.
“Uwekezaji huu mkubwa unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni, utafungua milango kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji. Tumeuweka uwanja huu kwenye mpango wa kimkakati wa maendeleo ya mkoa ili kuunganisha fursa zilizopo na masoko mapya, ndani na nje ya nchi,” amesema RC Mboni.

Amesisitiza kuwa, Serikali ya Mkoa itaendelea kuimarisha mazingira rafiki kwa uwekezaji, hasa kwa kuzingatia uwepo wa Kongani ya Kitaifa ya Biashara ya Buzwagi, ambayo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga, Lugano Mwinuka amesema mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na kazi kubwa zinazoendelea ni maboresho ya miundombinu ya kiufundi na kiusalama.
“Tunafanya ukarabati wa njia ya kurukia na kutua ndege (runway), maegesho ya ndege, jengo la abiria, mitaro ya maji, taa za usiku, uzio wa usalama na kituo cha hali ya hewa,” amesema Lugano.

Lugano ameongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutawezesha ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 74 kutua kwa urahisi. Hii ni hatua itakayopandisha hadhi ya kiwanja kutoka daraja la kwanza hadi la tano katika viwango vya zimamoto na usalama wa anga.
Naye kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Chiando Mwinuka, amethibitisha kuwa barabara kuu zote zinazounganisha uwanja huo na mikoa jirani kama Tabora na Mwanza tayari zimekamilika.
“Tumejenga barabara ya kisasa inayoingia moja kwa moja uwanjani. Lengo ni kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, na kuongeza ufanisi wa huduma za anga katika mkoa wetu,” amesema Mwinuka.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na Jambo Media kuhusiana na faida zitakazojitokeza baada ya kukamilika kwa uwanja huo akiwemo Ester Maziku mkazi wa Ngokolo na Tumaini Mabula mkazi wa Ibadakuli wamesema wana matumaini makubwa na kuinuka kwa uchumi wa mkoa wa Shinyanga kupitia uwanja huo.
“Zamani tulikuwa tukisafiri hadi Mwanza ili tupate ndege tena kwa kutumia muda mrefu lakini Sasa Uwanja tunao wenyewe, tunamshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha na kutuletea Uwanja wa Ndege na sasa tunaona kama tumeunganishwa na dunia. Hii ni fursa kwa wanawake wajasiriamali kama mimi,” amesema Ester.

Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga unatazamwa kama kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa kuzingatia utajiri wa rasilimali zilizopo mkoani hapa kuanzia ardhi yenye rutuba, madini, hadi vivutio vya utalii na uwekezaji.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu Tshs. Bilioni 52, ambapo asilimia 80 ya fedha zimetolewa na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya na asilimia 20 inagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania


