Rais Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika mwaka uliopita ni amani, ulinzi na usalama nchini kwa kuwa mipaka ya nchi ilikuwa salama.
Ameeleza mafanikio hayo katika sehemu ya salamu zake kwa Watanzania katika kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024.
Rais Samia pia Amegusia mapito ya kiuchumi duniani kutokana na UVIKO 19 na athari za vita yalisababisha mfumuko wa bei hususani wa chakula na mafuta ya vyombo vya moto na kuvuruga mnyororo wa ugavi wa kimataifa, kupanda kwa riba kwenye masoko ya fedha na kuathiri upatikanaji wa Dola za Marekani.
Amesema ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa mwaka jana ulikadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022 ambapo Serikali ilipokea Dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na shilingi trilioni tatu mwaka 2022/23 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo sawa na asilimia 100 ya kiasi kilichopangwa kukopwa.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Rais Samia amesema kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni mwaka jana, ukusanyaji ulifika Sh trilioni 22.6 sawa na ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2022, huku bajeti ya kilimo ikiongezeka kutoka Sh bilioni 751 mwaka 2022 hadi Sh bilioni 970 mwaka 2023.
Amesema kutokana na ushirikiano mzuri na nchi na mashirika ya kimataifa, Tanzania imefanikiwa kupata Dola za Marekani milioni 550 kwa ajili ya miradi ya usalama wa chakula, Dola milioni 297.64 za mradi wa mawasiliano vijijini, Chuo cha Teknolojia cha IIT Madras kutoka India na Dola milioni 500 kutoka Benki ya Dunia kusaidia bajeti ya Serikali.