Tume ya ulinzi wa taarifa binafsi (PDPC) imetoa mwezi mmoja kwa taasisi zote binafsi zilizopo hapa nchini kujisajili, ili kutunza taarifa za watu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Dkt. Emanuel Lameck amesema kitendo cha taasisi yoyote kutumia taarifa binafsi za mtu bila kujisali ni kinyume cha sheria na hatua kali zitachukuliwa kwa watakashindwa kutekeleza agizo hilo.

Katika hatua nyingine Dkt. Emanuel pia amewataka waandishi wa habari kuzingatia sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi katika uchapishaji wa habari.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usajili wa Tume hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe amesema tume ipo kwa ajili ya kumsaidia mwananchi yoyote endapo atabaini kua taarifa zake zimetumika vibaya na itasimamia malalamiko hayo kwa kipindi chote hadi mwananchi atakapopata haki yake.

Aidha Mhandisi Wangwe amesema kwa mujibu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi namba 11 ya mwaka 2022 zipo haki sita za mmiliki wa taarifa binafsi zinazotumika katika eneo au kampuni fulani ambazo anaweza kuzitumia kulinda taarifa zake.
Ametaja haki hizo kuwa ni pamoja na haki ya kuomba taarifa, haki ya kuzuia uchakati taarifa binafsi, kuzuia matumizi ya taarifa binafsi katika matangazo, kujua vigezo vya matumizi ya taarifa zinazochakatwa moja kwa moja, haki ya kulipwa fidia taarifa binafsi zikitumika tofauti.

Vilevile ametaja haki ya kudai taarifa binafsi kufutwa kama hazina matumizi tena ya msingi katika eneo au kampuni husika.
Aidha amesema endapo haki hizo zitakiukwa na taarifa binafsi zikatumika vibaya mhusika anayo haki ya kutoa malalamiko kupitia mfumo wa kidigitali wa PDPC na kuwa tume hiyo itasimamia na kugharamia mhusika apate haki yake.