Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imepiga marufuku utoroshaji wa madini unaofanywa na baadhi ya wachimbaji, ikieleza kuwa vitendo hivyo vinaathiri uchumi wa taifa na ni sawa na kuiua nchi yao wenyewe.
Marufuku hiyo imetangazwa leo Aprili 25, 2026 jijini Dodoma na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdullahman Mwanga, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa wachimbaji wadogo pamoja na wafanyabiashara wa madini, kwa niaba ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

“Mnapo torosha madini mjue mnatorosha mapato ya Serikali yenu, kwa maana Serikali itakosa mipango ya kuwasaidia nyinyi ikiwemo kuwapatia fedha ya kuendeleza miradi yenu kwa kuwa fedha hizo mnawapelekea wengine kwenye nchi zao,” amesema.
Aidha, amesisitiza suala la utunzaji wa Mazingira ambapo amesema wanapofanya shughuli za uchimbaji huku akiwahakikishia kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na mchango wa wachimbaji wadogo unaongezeka.

“Wizara itaendelea kuunga mkono jitihada zenu za uwekezaji kwenye utafiti, uchimbaji pamoja na kuhakikisha zinapatikana taarifa za utafiti kwenye maeneo mbalimbali ya uchimbaji mdogo ili kuwawezesha kuanzisha miradi yenye tija,”amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwase amesisitiza juu ya ushirikiano kwa wachimbaji ili kuhakikisha malengo ya sekta hiyo yanafikiwa.

“Madini hayachimbwi mdomoni bali yanachimbwa kwa vifaa, teknolojia na mtaji, kwenye magroup hivyo ndo vitu tunataka tuvione umegundua teknolojia mpya rusha kule tujadili,” amesema.
Naye rais wa shirikisho la wachimbaji Tanzania FEMATA, John Bina ameiomba STAMICO kutoa mafunzo kwa viongozi wa serikali za mitaa kwani hawajui sheria za uchimbaji madini jambo ambalo limekuwa likileta mkanganyiko baina yao na wachimbaji.

“Viongozi wetu wa serikali za mitaa nadhani hawajui sheria ya madini, wao nao wanasema wanaweza kugawa leseni wataibuka na kodi nyingi tu ambazo wanabuni wao, lakini wanaamini hii sekta watu wanapiga faida tu,” amesema.


