Na Daniel Gahu – Katavi.
Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Haidary Hemedy Sumry amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Mpanda ni kielelezo cha dhati cha namna ambavyo Serikali imesogeza huduma bora karibu na Wananchi.
Akizungumza na Wajumbe wa Baraza la wazazi wa CCM Wilaya ya Mpanda katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Mpanda kwa lengo la kuwashukuru kwa ushirikiano wao hadi kupelekea ushindi na kuwa mbunge wa Jimbo hilo la Mpanda Mjini, katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
Amesema, miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Barabara, Elimu, Kilimo, Maji pamoja na sekta nyingine umeongeza tija kwa wananchi kwa kusogezwa Kwa huduma hizo katika maeneo yao.

Aidha, katika Sekta ya Barabara ndani ya manispaa ya Mpanda amesema, ujenzi wa barabara wa kilomita 8.49 kupitia mradi wa TACTIC ambao utekelezaji wake umeanza kwa wakandarasi kuanza kujenga kambi kwaajili ya kuanza kutekeleza mradi huo utakaonufaisha baadhi ya kata na utakuwa ni mfano wa kuigwa kwa kujengwa Barabara za kisasa zitakazo upendezesha mji wa manispaa ya Mpanda.
‘’Katika hili namshukuru sana Rais wetu Dkt Samia suluhu Hassan mwanzoni kulikuwa na kusuasua kwa utiaji saini wa mkataba, lakini kabla ya uchaguzi wakati wa Kampeni Rais wetu alipokuja kuomba kura hapa Mpanda nilisimama na kumuomba kutia msukumo wa utiaji saini wa mkataba huo baada ya muda mkataba huo ulisainiwa na wakandarasi tayari wapo eneo la mradi na kazi inaendelea’’ anasema Haidary.

Katika hatua nyiningine, amewaomba wakazi wa Manispaa ya Mpanda kuupokea mradi huo wa barabara kwenye maeneo yao, pindi utakapo anza.
‘’Mkiwaona watalamu wetu wa ujenzi wa barabara wanaweka alama kwenye maeneo yetu huko tusishangae tufahamu ndio utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo umeanza,” amesema Haidary.
Katika sekta ya Maji amesema mradi wa maji wa Miji 28 unaojengwa katika Kata ya Shanwe ambao unagharimu zaidi ya Bilioni 22 unakwenda kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Mpanda pindi utakapo kamilika.

Mradi huo ambao umefikia asilimia 55 unakwenda kuwa mwarobaini wa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wanachi wa Manispaa ya Mpanda.
Katika Sekta ya Kilimo Haidary amesema serikali kuwekeza Bilioni 33 kwenye mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Kata ya Mwamkulu ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa kata hiyo na Manispa kwa ujumla.

‘’Tulifanya ziara katika eneo hilo la mradi wa umwagiliaji kiukweli mradi huo unaendelea vizuri na umefikia asilimia 70. Kukamilika kwa mradi huu wa umwagiliaji ni mapinduzi makubwa ya sekta ya kilimo kwa wanachi wetu wa Manispa ya Mpanda,’’ amebainisha Haidary.
Amewaomba Wanachi wa Manispaa ya Mpanda kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kwa kuwa maendeleo yanakwenda pamoja na umoja, amani na mshikamano.

Kikao hicho cha Wajumbe wa Baraza la Wazazi Wilaya Mpanda ni mwendelezo wa utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya wanachi unaoendelea kufanywa na Mbunge Sumry ambapo tayari ameshakutana na Wajumbe wa UWT Wilaya ya Mpanda, na leo anatarajia kukutana na wajumbe wa umoja wa Vijana UVCCM Wilaya ya Mpanda.