UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO SHINYANGA ULINGANE NA THAMANI YA FEDHA – MWAKISU

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Menejimenti  ya Manispaa ya Shinyanga ikiongozwa na muwakilishi wa Mkurugenzi, Jackson Mwakisu ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Rasilimali Watu Manispaa ya Shinyanga, wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua Miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ndani Manispaa hiyo.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na  Ujenzi wa Shule mpya ya Ishigwandama iliyopo Kata ya Kizumbi, ujenzi wa Madarasa mawili ya Shule ya Msingi Ilwelyangula Kata ya Kitangiri, ujenzi wa Ofisi ya Wajasiriamali Kata ya Lubinga na Ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Kambarage iliyopo katika Kata ya Kambarage.

Menejimenti hiyo, pia imtembelea na kukagua  Ujenzi wa Zahanati ya  Mwamagunguli iliyopo katika Kata ya Kolandoto, pamoja na ujenzi wa Mabweni manne na matundu ya vyoo 12 katika Shule ya Sekondari Rajani, iliyopo Kata ya Ibadakuli.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwakisu amewataka mafundi wanaotekeleza miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi, pamoja na kujenga majengo yenye ubora kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali, huku akisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia hatua iliyofikiwa pamoja na kuongeza nguvu katika maeneo yenye changamoto na kutoa ushauri, ili kukamilisha miradi hiyo.

“Ongezeni kasi ya ujenzi na uwe ujenzi wenye kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali ili majengo haya yaanze  kutumika kwa wanufaika wa miradi hii,” alisema  Mwakisu.

Nao baadhi ya Mafundi wanaotekeleza Miradi hiyo wamekiri kupokea maelekezo na kusema  watajitahidi kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *