Na Tryphone Odace, Buhigwe – Kigoma.
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya Buhigwe Mkoani Kigoma, limeeleza kuwa mabadiliko yanayoonekana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na majukumu ya Halmashauri yanaonesha hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa katika kuwahudumia wananchi.
Akizungumza katika katika kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Elles Gomwa alisema, Baraza hilo limeridhishwa na utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri, hususan katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri yetu inaendelea vizuri kwa sababu wataalamu wetu wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi” alisema Gomwa.
Aidha, Gomwa ameupongeza uongozi wa Halmashauri, akimtaja Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndug. George Emmanuel Mbilinyi, kwa usimamizi makini wa miradi ya maendeleo.

“Miradi ipo vizuri na wataalamu wanatekeleza majukumu yao vizuri. Buhigwe ya sasa siyo kama ya zamani, pongezi nyingi ziende kwa Mkurugenzi wetu,” amesema Gomwa.
Hata hivyo, Baraza la Madiwani limeeleza kuwa utekelezaji mzuri wa majukumu pamoja na usimamizi madhubuti wa miradi vinaendelea kuchangia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hatua hizo zimeendelea kuongeza kasi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, huku ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu na wananchi ukiwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo.
Mabadiliko yanayoonekana katika utekelezaji wa miradi Mkoani humo, yanaendelea kutoa matumaini ya kuimarika zaidi kwa huduma na miundombinu katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe.


