Jambo La Leo

Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Utata kuhusu kifo cha Nisher

Chanzo cha kifo cha mtayarishaji wa video za muziki wa kizazi kipya, Nick Davie maarufu Nisher kimeibua utata kutokana na kile kinachodaiwa alitaka kujiua.

Nisher inaelezwa alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali binafsi ambayo hata hivyo, haijawekwa wazi.

Habari zinasema mwili wa Nisher utaagwa katika Nyumba ya Matamko iliyopo Kisongo, wilayani Arumeru.

Eneo hilo ndipo baba wa Nisher, Nabii Dk GeorDavie huendesha mahubiri katika kanisa lake la Ngurumo za Upako.

Akizungumza na Mwananchi  Digital leo Jumanne Desemba 12, 2023, Msaidizi wa Nabii huyo, Apostle Sekela amesema maziko yatafanyika Jumamosi Desemba 16,2023 na shughuli zote za kuaga mwili zitafanyika katika Nyumba ya Matamko, Kisongo.

“Suala la chanzo cha kifo familia itaeleza lakini ninachojua mimi amefariki dunia usiku hapa Arusha,” amesema.

Akuzungumza na Mwananchi Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema wameanza uchunguzi kujua chanzo cha kifo cha Nisher.

“Na mimi nimepata taarifa za kifo cha huyu msanii kupitia vyombo vya habari, tunafuatilia. Uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa,” amesema.

Taarifa iliyothibitishwa na Nabii Geordavie inasema Nisher amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Desemba 12, 2023 jijini Arusha.

Peter Msoffe, mmoja wa marafiki wa Nick, amesema alichoelezwa ni kuwa alikuwa anaumwa kutokana na majeraha baada ya kutaka kujiua.

“Nick alikuwa na msongo wa mawazo kutokana na kutofautiana na mke wake. Tulielezwa alitaka kujiua kwa kujikata, hatukuwahi kumuona hadi mauti yamemfika,” amesema.

Baadhi ya wasanii katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam waliowahi kufanya kazi na Nisher wamekuwa wakitoa salamu za pole kwa msiba huo.

Msanii Shabani Juma, maarufu Shah Bang amesema ni siku ya huzuni kwake baada ya kupata taarifa za msiba wa Nisher, kwa sababu ndiye alikuwa msanii wa kwanza kumshirikisha.

“Nisher tulishirikiana kwenye wimbo wangu ulioitwa ‘Maisha ya ujana’ ulifanyika Bongo Records kwa mtayarishaji P. Funky Majani. Nisher ndiye aliyetayarisha video ya wimbo ambayo ndiyo ilimtambulisha katika tasnia ya muziki Tanzania,” amesema.

Amesema baada ya video ya wimbo huo kutoka, alikutana na msanii Joh Makini aliyeipenda video hiyo, hivyo alienda Arusha kufanya naye kazi ya video ya wimbo ulioitwa ‘Sijutii’ na ndiyo ukawa mwanzo wa Nisher kupata umaarufu.

“Baada ya hapo alifanya video nyingi ambazo zilifanya vizuri ndani na nje ya nchi, kwa hiyo kifo chake ni pigo kubwa katika tasnia ya muziki wa Arusha na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

Amesema Nisher alikuwa na kipaji cha kuandaa video za muziki na alikuwa na ndoto za kuwa mwandaaji bora wa muziki.

Msanii mwingine, Jordan Peter amesema wamepoteza mtu muhimu katika tasnia ya muziki, ambaye alifanya uwekezaji mkubwa katika kazi zake.

Maandalizi ya shughuli za kuaga mwili yanaendelea kanisani Kisongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *