Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amezitaka Mamlaka, Taasisi, Asasi za Kiraia na Vikundi mbalimbali kufanya kazi kwa kushirikiana, ili kuondoa changamoto ya magugu maji Katika Ziwa Victoria
Ameyasema hayo alipotembea eneo la Kigongo Busisi wakati kukagua maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu utekelezaji wa utoaji wa magugu maji Katika ziwa Victoria, hususani katika eneo la Kigongo Ferry ambayo yamekuwa kikwazo kwa wasafiri na wavuvi.

“Hapa kuna athari mbalimbali na sote tunahitajika katika kufanya usafi ziwani, hii shughuli sio ya Bonde tu bali Taasisi na Wizara zingine zinaweza kuathirika lazima muwekeze fedha ili shughuli hii iende vizuri”.
Katika hatua nyingine Mtanda pia ameishukuru serikali kwa kutoa fedha ya dharura kiasi cha shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha huduma katika ziwa viktoria na kupitia fedha hizo imefanikisha ununuzi wa mtambo wa uvunaji wa magugu maji katika ziwa Victoria.

“kuwa na mashine ya kisasa ya kufyeka magugu halikwepeki kwa taifa linalotaka maendeleo na kutatua changamoto hii kwa muda mrefu hivyo tunaipongeza sana Serikali”.
Kwa upande wake meneja wa bodi ya maji bonde la ziwa Victoria Revictus Shinhu amesema mpaka sasa tayari tani 441 za magugu maji yameopolewa na shughuli hiyo inaendelea ikiwa ni mpango wa muda mfupi mpaka pale mtambo wa kuvuna magugu maji utakapofika.

Aidha pia amesema kwa kushirikiana na ofisi zingine wameandaa andiko Kwa wizara ya fedha ili kupata kiasi Cha billion 3.1 tsh ili kushughulikia Changamoto hiyo Kwa kununua mtambo wa kuondoa magugu hayo.
Itakumbukwa kua athari za magugu maji zilianza kuonekana mwezi wa kwanza Mwaka huu ambapo gugu maji hilo lilianza kuleta athari mbalimbali kwenye sekta ya uvuvi, ufugaji samaki (Vizimba-Luchelele na Bukumbi).

Aidha, iliathiri pia vyombo vya usafiri hususani vivuko katika eneo la Kigongo-Busisi na kuzorotesha huduma ya usafiri kati mkoa wa Mwanza na mikoa ya karibu ambayo inatumia vivuko.