USHETU: WAZAZI WASIOCHANGIA CHAKULA SHULENI KUITWA KIKAO

Na William Bundala, Ushetu – Kahama.

Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata wa Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, wameagizwa kufanya vikao na wazazi wasiochangia chakula shuleni ili waweze kuchangia, ili watoto wao wapate chakula wawapo shuleni.

Agizo hilo limetolewa na Afisa Elimu Sekondari, Emmauel Malima katika kikao cha lishe kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa hospitali ya wilaya ya Ushetu  baada ya kubainika kuna baadhi ya wanafunzi hawala chakula kutokana na wazazi wao kutokuchagia.

Amesema, “niwaombe sana wakuu wa shule Pamoja na maafisa elimu kata,wekeni mikakati na vikao kuhakikisha mnafanya vikao na wazazi ambao hawachangii chakula kwa ajili ya watoto wao,hili swala haliwezekani mana kama wangekuwa hawasomi bajeti yao nyumbani si ipo tu sasa kwanini wanashindwa kuchangia.”

Kwa mujibu wa Afisa Elimu Sekondari, Emmanuel Malima amesema Shule zote za Sekondari Halmashauri ya Ushetu, Wanafunzi wanapata chakula shuleni, isipokuwa kuna baadhi yao hawapati kutokana na wazazi wao kutochangia.

“Ndugu Mwenyekiti katika Halmashauri yetu takribani shule zote za Sekondari Wanafunzi wanapata chakula,isipokuwa wapo wanafunzi wachache wasiopata chakula kutokana na wazazi wao kutochangia huduma hiyo,” ameongeza Malima.

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi na Awali, Bi. Velena Ntulo amesema zaidi ya asilimia 98 ya shule zote za Msingi na awali, watoto wanapata chakula shuleni, na wanaendelea na kuhamasisha jamii ili kuwezesha upatikanaji wa chakula kwa 100% mashuleni.

“Kwa upande wa shule za msingi na awali,zaidi ya 98% watoto wanapata chakula tuna asilima 2 tu ambao hawapati chakula tunaendelea kuhamisha jamii na wazazi ili kuwezesha upatikanaji wa chakula kwa 100% mashuleni,” amesema Ntulo.

Katika kikao hicho, Divisheni ya Elimu Sekondari imeshauriwa kuweka mipango madhubuti na njia bora za kuhifadhi chakula mashuleni, kwani pamekuwa na changamoto ya kuhifadhi chakula kwenye shule nyingi za Upili.

Kikao hicho hicho kilihudhuliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe mbalimbali na wadau wa elimu  kikiwa na lengo la kujadili maswala muhimu yanayohusu lishe na kuweka mikakati yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa lishe bora kwa  shule za halmashauri ya Ushetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *