Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Halimashauri ya wilaya ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa jumla ya mitungi 50 ya gesi kwa akina mama lishe pamoja na wanawake wanaoishi na ulemavu.
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati nyingine zisizo salama zenye kuharibu mazingira kama vile kuni na mkaa na kuhamia katika nishati safi za kupikia kwa ajili ya kulinda afya na mazingira katika jamii husika.
Akizungumzia suala hilo mratibu wa nishati safi katika halimashauri ya Ushetu Naomni Mbelwa amesema halimashauri hiyo imeendelea kujipanga kutoa elimu kwa wananchi katika kata zote 20 na vijiji vyake kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema hatua hiyo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi na kuendelea kulinda misitu na mapori ya akiba yaliyipo katika halimashauri hiyo.
Mbelwa ameongeza kuwa kati ya mitungi 50 iliyogawiwa,mitungi 25 imenunuliwa kupitia mapato ya ndani ya halimashauri ya Ushetu,huku mitungi 30 ikitolewa na wadau wanaoshrikiana na halimashauri hiyo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Sisi kama halimashauri tumejipanga kutoa elimu kwenye kata zote20 na vijiji vyake kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii nzima ya wana Ushetu”amesema Mbelwa.
Nae mmoja wa wanufaika aliyepatiwa jiko la gesi Eva Maziku kutoka kata ya Kinamapula amesema kupatiwa jiko hilo kwake ni faida kwani itamsaidia kupunguza gharama za kununua mkaa na kwamba atalinda afya yake na mazingira kwa ujumla.
Amesema Awali alikuwa akitumia gunia moja la mkaa kwa wiki ambalo lilimgharimu kati ya shilingi 25000 hadi 30000 hivyo kwa kupata jiko hilo itampelekea kuokoa kiasi cha pesa nyingi kwa mwezi na kwamba atakielekeza katika matumizi mengine.
“Kwa kupata majiko jiko hili nitakuwa tayari nimetunza mazingira na pia afya yangu hivyo mimi kama mama namshukuru sana Dr Samia Suluhu Hassan rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutuona sisi kina mama lishe wa Ushetu abarikiwe sana”amesema Maziku.
Kwa upande wake Lucia Shija mama lishe mwenye ulemavu wa viungo amesema matumizi ya gesi kama nishati safi ya kupikia yatamuepusha na adha ya kutafuta kuni porini jambo ambalo kwake lilikuwa gumu kutokana na hali yake ya ulemavu.
Amesema anaishukuru serikali kwa kuwakumbuka pia watu wenye ulemavu katika mpango wa nishati safi ya kupikia kwani mara nyingi jamii imekuwa ikiwasahau katikamambo mbalimbali.
“Kwa kweli tunashukuru mimi nilikuwa natumia kuni kwa kukata kwenye mapori huko na ukija kupika moshi unakuwa mwingi macho yanakuwa mekundu mpaka tunaitwa wachawi ,lakini sasa hivi nitapika vizuri”amesema Lucia
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kulinda afya na mazingira na kupunguza uharibifu wa misitu hivyo ni dhima ya serikali kuwa kila mwananchi atumie nishati safi ya kupikia.


