Na William Bundala, Ushetu – Kahama.
Wakulima halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga,wametakiwa kutumia mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo kupalilia na kuweka mbolea ya kukuzia kwenye mashamba yao ili kuwahi unyevu uliopo ardhini.
Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Ushetu, Mapenzi Mshana wakati akizungumza na Jambo Fm ilipotembelea katika halmashauri hiyo kuona shughuli za kilimo kufuatia mvua kunyesha siku ya jana.
“Tunashukuru jana December 9 tumepata mvua ya kutosha katika halmshauri yetu ya Ushetu,Sasa nitoe wito kwa wakulima watumie mvua hizi zilizonyesha kufanya palizi katika mashamba yao Pamoja na kuwekea mbolea ya kukuzia katika mazao yao,” amesema Mshana.

Sambamba na hayo amewataka wakulima waliopanda maharage na yakaunguzwa kwa jua kutumia mvua hizo kurudia kupanda maharage kwani zao hilo halichukui muda mrefu kustawi.
“Kwa wale wakulima ambao walipanda maharage na yameungua na jua nawashauri warudie tena kupanda maharage kwani maharage yanachukua muda mfupi na yatakomaa kwa wakati” Amesisitiza Mshana.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamilangano Charles Nkwabi ametoa wito kwa wananchi kutumia mvua zilizonyesha kufanya kazi za mashambani na kuacha kukaa vijiweni kwani serikali ya awamu ya sita imeleta pembejeo za kutosha na kwa bei nafuu ya ruzuku.

“Mimi kama kiongozi nitoe wito kwa wananchi wa kata ya Nyamilangano kutumia mvua hizi kufanya kazi mashambani,niwasihi waache kukaa vijiweni kucheza karata ,watumie fursa hii Kwenda shambani na mbolea zipo kwa bei nzuri ya ruzuku” Amesema Nkwabi.
Nao baadhi ya wakulima Juma Nzamal ana Shija Mathew wamesema kuwa wanashukuru Mungu kwa kunyesha mvua hiyo na kwamba watazingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo ili kukuza uzalishaji wa mazao yao ambayo yalikuwa hatarini kuungua.

“Tunashukuru Mungu kwakweli kwa kunyesha hii mvua japo upande wa maharage hatuna matumaini ila kwa mahindi walau matumaini yapo,tunashukuru afisa kilimo wetu bwana Mshana kwa kutupa matumaini na meelekezo,tutayafanyia kazi ili kuhakikisha tunakuza uzalishaji wa mazao yetu” Wamesema Wakulima hao.
Halmsahauri ya ushetu jana imepata mvua ya kutosha baada ya wiki mbili kuwa na jua kali huku mazao kama Tumbaku,Mahindi,Karanga na Maharage yakiwa yamepandwa na kudhohofika na hali ya ukame.


