Serikali Nchini, imesema inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Mikoa ya Singida na Dodoma unaotarajiwa kukamilika Mwezi Juni, 2025.
Akizungumza leo Aprili 14,2025 Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Maji, Mha. Andrew Kundo wakati akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga ambapo ameuliza Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha Vijiji vyote vya Mkalama vilivyopo umbali wa Km 20 litakapopita bomba la Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria vinapata maji.
Amesema, “Mradi huo utakapotekelezwa unatarajia kuhudumia miji ya Singida na Dodoma pamoja na vijiji vilivyo ndani ya umbali wa kilomita 12 kutoka kila upande wa bomba kuu ikiwemo vijiji vya Wilaya ya Mkalama.”
“Aidha, vijiji vitakavyokuwa nje ya kilometa 12, Serikali itavipelekea huduma ya mradi wa Ziwa Victoria baada ya awamu ya kwanza ya mradi huo kukamilika na kuanza kutoa huduma,” amesema Muhandisi Kundo.

Hata hivyo, amesema kwa sasa jumla ya vijiji 29 kati ya 70 vya Wilaya ya Mkalama vinapata huduma ya majisafi na salamakupitia mtandao wa bomba wakati vijiji 41 vinapata huduma ya maji kupitia point source na pampu za mkono.
“Serikali inaendelea na utekelezaji wa jumla ya miradi Sita (6) ya Mbigigi, Isene-Matongo, Mdilika, Tumuli, Singa naMwangeza ambapo kukamilika kwake kutanufaisha wananchi zaidi ya 15,000 waishio kwenye vijiji Saba (7) vya Wilaya ya Mkalama”, amesema
Vilevile amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Maji Vwawa-Mlowo pamoja na Mradi wa Ukarabati wa Vyanzo vya maji Mwansyana na Mlowo.
“Utekelezaji wa mradi wa Vwawa-Mlowo umefikia wastani wa asilimia 79 wakati mradi wa ukarabati wa Mwansyana-Mlowo umefikia wastani wa asilimia 94 na tayari baadhi ya maeneo ya Mlowo Forest, Izyla, Saganoti, Malenje, Segerea, Mbimba, Ilolo Shule na Namleya yameanza kupata huduma ya maji kupitia miradi hiyo”, amesema
“Mheshimiwa Spika, Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2025 na kunufaisha wananchi 36,744 waishio kwenye maeneo ya Hasamba, Ilolo, Vwawa, Ichenjezya, Mlowo Mabatini, Mlowo Mjini, Tazara, Kiwandani, Ichenjezya, Isangu, Hasanga, Mlowo Forest, Izyla, Saganoti, Malenje, Segerea, Mbimba, Ilolo Shule na Namleya”. Amesema Muhandisi Kundo

