Serikali imeweka maelekezo kwa kila Shule kutenga chumba maalum cha Wasichana maalum kwa ajili ya kujisitiri wakati wa hedhi na kwamba mwongozo wa uanzishaji na Usajili wa Shule (2020) umetoa maelekezo hayo kuwa ni miongoni mwa kigezo cha usajili wa shule.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Amina Mzee ambapo ameuliza Je? lini suala la Hedhi Salama litapewa kipaumbele kwa kugawa taulo za kike bure katika Shule za Msingi na Sekondari na kuboresha miundombinu ya Vyoo.

Amesema, “Serikali inatekeleza Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Shuleni ambao umeweka maelekezo ya kila shule kutenga chumba kwa ajili ya kubadilishia sambamba na Mwongozo wa Usanifu wa Miundombinu ya hedhi ambayo ni chumba cha kubadilishia ambacho kimeunganishwa na kiteketezi.”
Dkt Mollel ameongezea kuwa Serikali ilishaanza kutekeleza mpango wa hedhi salama katika shule za msingi na Sekondari kwa kutoa elimu juu ya masuala ya hedhi kwa lengo la kuvunja ukimya, uwekaji wa miundombinu ya kudhibiti bidhaa za hedhi, kuhakikisha watoto wa kike wanapata bidhaa bora na salama wakati wa hedhi pamoja na utoaji wa msaada wa kijamii ambapo baadhi wamekuwa wakipata maumivu makali wakati wa hedhi.