Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Athumani Mwiniko, limefanya mkutano maalum katika ukumbi wa Halmashauri, kwa ajili ya kujadili taarifa ya ufungaji wa hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Halmashauri ya Wilaya ya Urambo Bw. James Kulugendo, amesema hesabu hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia mfumo wa kimataifa wa uandaaji na ufungaji wa hesabu za sekta ya umma (IPSAS) na zinatarajiwa kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haraka iwezekanavyo kwa ajili ya ukaguzi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bw. Sadoki Magesa, amesema taarifa hiyo ni muhimu kwa Halmashauri kwa kuwa itawasilishwa kwa CAG na kupitia ukaguzi huo Halmashauri inatarajia kupata hati nzuri inayostahili.
Aidha, wajumbe wa Baraza wamepongeza uandaaji wa taarifa hiyo huku wakisisitiza umuhimu wa Halmashauri kuhakikisha miradi yote viporo ambayo haijakamilika inamaliziwa, ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo.

Wajumbe pia wameitaka Halmashauri kuhakikisha makampuni na taasisi zote zinazodaiwa fedha zinalipa madeni yao kwa wakati, ili fedha hizo zitumike katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Halmashauri.






