Urambo, Kaliua na Uyui Umeme Utamwagika, Mradi Wafikia 92%

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mha. Gissima Nyamo-Hanga ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa kituoa cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Uhuru – Urambo (Kilovolti 132) mkoani Tabora ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt Doto Biteko aliyoyatoa Machi 27, 2024 alipotembelea mradi huo na kusisitiza usimamizi wa karibu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa .

Mhandisi Gissima amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huu utakwenda kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika wilaya za Urambo, Kaliua na Uyui ambapo itapelekea wananchi kupata huduma bora ya umeme kwasababu mradi huo ni mahsusi kwaajili yao kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili waweze kufurahia matunda ya juhudi ambazo serikali inafanya kuhakikisha wanapata umeme .

Akieleza hatua iliyofikiwa mara baada ya kufanya ukaguzi huo Mhandisi Gissima amesema kuwa Dkt Doto Biteko alipotembelea kituoni hapo ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 84 lakini katika kipindi cha miezi miwili kutoka mwezi Machi mwishoni mpaka sasa ujenzi umefika asilimia 92 na hivyo kufanya ongezeko la asilimia 8.
Kwa upande wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme amesema kuwa Dkt. Doto Biteko aliwataka ETDCO waongeze jitihada kuhakikisha kasi yake inaendana na ujenzi wa kituo ambapo kwasasa umefikia asilimia 25 kutoka asilimia 10 za Mwezi Machi,2024.

Utekelezaji wa mradi huu ulianza 18, Septemba, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024 ambapo kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza imegawanyika katika sehemu mbili ya ujenzi wa kituo ambao unafanywa na kampuni ya TBEA kutoka China huku kazi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Urambo (Km 115) ikifanywa na kampuni ya ETDCO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *