Na Costantine James,Geita
Imeelezwa kuwa moja ya changamoto kubwa inayopelekea kuongezeka kwa mmonyoko wa maadili hasa kwa vijana hapa nchini pamoja na matukio ya ukatili kwa vijana ni upendo uliopitiliza wa wazazi na walezi kwa watoto wao hali ambayo imekuwa ikisababisha wasahau kutekeleza majukumu yao ya malezi na kupelekea vijana kujiingiza katika makundi na tabia hatarishi zinazosababisha vijana kuharibika kimaadili.
Hayo yamebainishwa leo juni 11,2024 na baadhi ya wazazi na walezi walioshiriki katika semina kwa vijana kuanzia miaka 10 hadi 35 iliyotolewa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Jodade Foundation iliyofanyika mjini Geita na kuwakutanisha vijana kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambapo wamesema uwepo wa hali ya wazazi kuzidisha upendo badala ya malezi imekuwa chanzo cha wao kushindwa kuwaonya watoto wao pale wanapokengeuka.
Mkurugenzi wa Jodade Foundation Jesca Lumanyika amesema kutokana na changamoto zilizopo hivi sasa ndani ya jamii hasa kwa upande wa malezi kwa vijana,shirika hilo limelazimika kutoa elimu ya kujitambua kwa vijana kuanzia miaka 10 hadi 35 ili kuwajengea uelewa zaidi hasa kitika maswala ya teknolojia kwa kujua madhara yake na faida ili kujenga vijana wenye maadili bora katika taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba, afisa tarafa ya Geita Cosmas Bayaga amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa vijana kwani yamelenga zaidi kuwawezesha vijana kujitambua kwani vijana wengi hawajimbui hali ambayo inasababisha vijana kufanyiwa matukio ya ukatili na kushindwa kutoa taarifa mapema mahala husika.
Nao baadhi ya vijana kutoka katika mikoa mbalimbali hapa nchini walioshiriki semina hiyo wamesema imekuwa muhimu kwao kwani imewajengea uwezo wa kutosha katika kujitambua pamoja na kujiepusha na matukio ya unyanysaji wa kijinsia ambayo vijana wengi wamekuwa wakifanyiwa kutokana na kukosa elimu sahihi juu ya madhara ya matukio hayo.