Habari hii inaonyesha na kutufunza jinsi ‘uamuzi usio na ubinafsi wa mtu mmoja unavyoweza kuleta mwanga kwenye ulimwengu wa mtu mwingine’ kauli ambayo ilitolewa na Meena Mehta wa India.
Ipo hivi: Mchoraji mmoja Raj Kumar (sio jina halisi), wa Nchini India alipoteza mikono yote miwili katika ajali mbaya ya treni mwaka wa 2020 na katika miaka minne aliishi akiwa na hali hiyo bila tumaini jipya.
Lakini jambo la kushangaza lilitokea baadaye kwani Mkuu wa Utawala wa Shule maarufu Kusini mwa Delhi, mwanamama Meena Mehta alitangaza kutoa viungo vyake kwa wahitaji mara atakapokufa.

Alitoa tangazo hili baada ya kukutwa na maradhi ya Ubongo na familia yake iliheshimu matakwa yake, habari ambayo ilibadilisha kila kitu, na kumpa msanii yule aliyepoteza mikono nafasi ya kuchora tena.
Januari 2024, Madaktari katika Hospitali ya Sir Ganga Ram walifanikisha kile ambacho kilionekana kuwa hakiwezekani baada ya kufanikisha uandikizaji wa kwanza wa mikono jijini New wa Delhi na India Kaskazini.
Hii ilikuwa ni moja ya upandikizaji adimu uliofanywa kwa mtu aliyepoteza mikono kwenye ajali na aliruhusiwa kwa mafanikio Machi 2024, akionesha dole gumba kuashiria maendeleo yake.

Upasuaji huo ulitajwa kuwa mgumu sana, na ulidumu kwa saa 12 huku ukibatizwa jina la ‘upasuaji wa muujiza’ ukihusisha kuunganisha kila mshipa wa damu, misuli, na neva kati ya mikono ya mtoaji na mikono ya mpokeaji.
Hapa inatukumbusha kwamba hata katika wakati wetu wa giza zaidi, matumaini yanaweza kutoka kwa sehemu zisizotarajiwa, kwani wakati mwingine, kazi ni bora zaidi sio kwa kile tunachounda bali urithi tunaochagua kuwaachia wengine.