UONGOZI HAUPIMWI KWA MANENO BALI VITENDO – KUNDO

Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.

Zikiwa zimebaki takriban siku 11 watanzania waamue kwa kupiga kura kumchagua kiongozi atakayewavusha ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, Viongozi wa vyama mbalimbali ya siasa wameendelea kumwaga sera zao zenye ushawishi kwa wapiga kura wao.

Jimbo la Bariadi mjini Mkoani Simiyu,   mpeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM), nafasi ya Ubunge Injinia Kundo Andrea, ameendelea kuzinadi sera za katika mtaa wa Izunya, Nyaumata na Bipyai, huku akiwataka wanachi hao kumpima kiongozi kwa matendo na si maneno.

“Mambo ambayo CCM imeyafanya yanaonekana hakuna porojo na mtu yeyote haambiwi tazama hayo mnayoyaona ndiyo matunda ya kuchagua viongozi makini ambao vitendo vyao vinaonekana,” amesema injinia Kundo.

Akihutubia Wananchi, Kundo amewahakikishia kuwa changamoto ya huduma ya maji safi na salama ambayo wamekuwa nayo kwa muda mrefu inakwenda kumalizwa na mradi wa Ziwa Victoria na kwa wale wasio na uwezo wa kuvuta huduma hiyo majumbani, utaratibu wa kuwapatia pampu za kuvuta maji utafanyika, ili wapate huduma hiyo.

“Bilioni 440 zinatumika katika kuleta maji ya mradi wa Ziwa Victori ambao unakwenda kabisa kumaliza shida ya maji kazi yenu inakuwa kuvuta maji tu na ninatambua zipo kaya ambazo zitashindwa kumudu gharama za kuvuta maji niwahakikishie lengo letu ni kumtua mama ndoo kichwani basi tutawapatia pampu ili zitumike kuwasogezea maji, ili kusiwe na kaya ambayo haina huduma hiyo,” ameongeza Injinia Kundo.

Kuhusiana na suala la changamoto ya umeme Kundo amesema kwa sasa kumeanza utekelezaji wa mpango wa Compact Mission 300, ambao unakwenda kumaliza tatizo la umeme.

“Hakutokuwa na maendeleo kama hakuna umeme ambao utaleta ajira kwa vijana ,na kufungua mipaka ya kibiashara kitu pekee unachotakiwa kufanya nikuhakikisha umesuka umeme ndani ya nyumba yako ili wakija kuweka umeme wakute kila kitu kipo sawa hiyo ndiyo Compact Mission 300,” aliongeza Kundo.

Aidha, amegusia maboresho ya huduma za afya akisema watamalizia ukarabati wa Zahanati ya Bipyai kata ya Nyangokolwa pamoja na kuboresha miundombinu ya elimu kwa manufaa ya wananchi wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *