Ikiwa imepita siku moja baada ya bunge la umoja wa ulaya (EU) kutaka uchunguzi huru ufanyike dhidi ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa wilaya za Ngorongoro na Loliondo Mkoani Arusha,serikali imesema wataalam wa shirika la UNESCO watakwenda kufanya ukaguzi katika maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na msemaji mkuu wa serikali Mobhare Matinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali ilivyo hanang mkoani Manyara na kwa wananchi wa Ngorongoro.
Katika hatua nyingine Matinyi ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwahudumia waathirika wa maporomoko ya udongo Hanang ambapo wataalamu wa afya wanaendelea kutoa huduma huku kati ya majeruhi 139 wawili ndiyo waliopoteza maisha na 14 wamesalia katika hospitali baada ya wengine kuruhusiwa.
Ikumbukwe kuwa maporomoko hayo ya udongo mji wa katesh wilayani Hanang mkoani Manyara yalitokea Desemba 3 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 89.