UNAPOTOA MSAADA USIANGALIE IMANI YA MTU – SHEIKH KWEZI

Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.

Mlezi wa shule ya msingi Bariadi ambaye pia ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Sheikh Issa Kwezi ameitaka jamii mkoani humo kutoangalia imani ya mtu pale anapotaka kutoa msaada kwani kwa kufanya hivyo atakuwa anaijenga jamii salama na yenye upendo.

Kwezi ameyasema hayo katika hafla fupi na ya makabidhiano ya Jokofu kwa shule ya Msingi Bariadi iliyopo mjini Bariadi, kwa ajili ya matumizi wa Walimu ikiwa ni katika kutimiza ahadi zake kama mlezi wa shule hiyo.

Amesema, “mlikuwa na maombi kwangu ambayo ni kupata jokofu na kuwekewa samani za ofisi na mimi kama mlezi nimeanza kutimiza hili na lingine litafuata hapo baadae,hili liwe somo kwetu kwamba upendo hautakiwi kuangalia imani ya mtu pale unapotakiwa kutoa kwa kufanya hivyo kutajenga jamii salama,watakao tumia jokofu hili ni walimu wa dini zote kwa sababu sisi sote ni wa moja na tunaishi mara moja.”

Aidha, Sheikh Kwezi amewataka Walimu kuzingatia kanuni na maadili ya kazi yao na kutojiingiza katika nafasi itakayo waharibia ajira zao hususan kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.  

“Tupo kwenye kipindi cha uchaguzi tujihadhari na kauli zetu na matendo yetu tusijiingize kwenye harakati zikaathiri ajira zetu maana wapo ambao hawana ajira huko nje chungeni msizichezee,” ameongeza Sheikh Kwezi.

Akipokea Jokofu hilo, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Hamza Saire amemshukuru mlezi huyo huku akiahidi kuendelea kushikana mikono kwa juhudi na maarifa katika kuleta matokeo mazuri kwa watoto wa shule hiyo, ili wajiendeleze na si tu kuwafundisha kujua kusoma na kuandika.

“Ulituasa na kutuomba kujitahidi kutimiza azma ya serikali ya amani na upendo muda wote,ushirikiano mzuri na jamii pamoja na kuwapa elimu bora watoto wetu na hayo tumetimiza tunafanya kazi saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni ili mtoto atoke hapa si tu ajue kusoma na kuandika bali afaulu kwa ngazi zote,” amesema Hamza.

Naye afisa elimu kata ya Malambo Bi Lilian Kagirwa amewataka walimu hao kuthamini na kutunza mchango wowote unaotolewa shuleni hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *