UN yataka Uchaguzi Sudan Kusini

Umoja wa Mataifa umevitaka vyama vyote vya siasa nchini Sudan Kusini kuchukua hatua za haraka ili kuruhusu uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu unafanyika mwishoni mwa mwaka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa ripoti inayoeleza kwamba ni muhimu vyama vyote vya siasa nchini Sudan Kusini kuchukua hatua za dharura katika kufanikisha mchakato wa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika.

Taarifa hiyo ya Guterres imeeleza kuwa baada ya tathmini ya hali jumla, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umehitimisha kuwa wadau wote bado wanahitaji msaada wa haraka katika masuala ya utaalamu, sheria na uendeshaji kwa ajili ya kuandaa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu au baadaye.

Guterres ameeleza kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa shughuli na masharti muhimu yanayohitajika kabla ya kufanyika uchaguzi na kusisitiza kwamba itakuwa changamoto kubwa kwa taifa hilo masikini kuandaa kwa siku moja uchaguzi wa kitaifa, wa majimbo na serikali za mitaa.

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo ilitangaza wiki iliyopita shughuli za kuwaandikisha wapiga kura ingelianza mnamo mwezi Juni lakini  Guterres amesema viongozi wa Sudan Kusini wameafiki kwamba kuenea kwa ghasia katika baadhi ya maeneo madogo nchini humo kunaleta changamoto katika uendeshaji wa uchaguzi.

Sudan Kusini haijafanya uchaguzi tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, na taifa hilo limekuwa likikumbwa na mizozo ya kila mara, umasikini uliokithiri na majanga ya asili pia mipango ya uchaguzi imevurugwa na mabishano makali baina ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake mkuu, Riek Machar, ambaye kwa sasa ndiye makamu wa rais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *