Na Costantine James,Geita
Jeshi la polisi Mkoa wa Geita limetoa tahadhari kwa wazazi na walezi mkoani humo kutokana na kuibuka kwa wimbi kubwa la matukio ya ulawiti kwa watoto wa kiume katika wilaya za mkoa huo hali ambayo inahatarisha usalama wa watoto kutokana na matukio hayo kuongezeka .
Hayo yamebainishwa leo Mei 15,2024 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Safia Jongo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ihushi kata ya Shabaka wilaya ya Ng’wale Mkoani Geita katika ziara ya mkuu wa mkoa wa Geita ambapo amefafanua kwamba ongezeko la vitendo hivyo vya kikatili limechangiwa na utandawazi pia wazazi na walezi kushindwa kuwajibika vyema katika malezi.
Wakati huo huo kupitia ziara hiyo ya mkuu wa mkoa wa Geita, Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amesema moja ya changamoto iliyopo katika kata ya Shabaka ni baadhi ya wananchi kujihusisha na kilimo cha bangi na kutumia fursa hiyo kupiga marufuku shughuli hiyo haramu na kuwataka wananchi kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwemo kuachana na kilimo cha mihadarati.
Aidha akizungumza na wananchi kupitia ziara yake hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ameuagiza wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Geita kuhakikisha wanachimba kisima haraka katika kata ya Shabaka ili kuwaondolea wananchi changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.