Na William Bundala, Kahama – Shinyanga.
Serikali Wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, imewataka wachimbaji wadogo wa madini kuwekeza katika amana za muda zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania(BoT), ili kujiwekea akiba ya baadaye na kukuza mitaji yao.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda wakati akifungua mafunzo ya programu ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara, yaliyoandaliwa na Benki ya Tanzania Tawi la Mwanza.

Nkinda amesema wachimbaji wengi bado hawana utamaduni wa kuwekeza kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi, jambo linalokwamisha ukuaji wa mitaji yao.
“Suala la uwekezaji ni muhimu kwa ndugu zetu wachimbaji,wengi hatuna utamaduni wa kuweka amana,jambo hili linakwamisha ukuuji wa mitaji yetu na wakati mwingine kushindwa kuwa na akiba ya baadae,” amesema Nkinda.

Amesema elimu inayotolewa itakuwa chachu ya mafanikio kwao, huku ikiwasaidia kuachana na tabia ya kutembea na fedha taslimu na badala yake kuhamia katika mifumo salama ya kifedha.
“Elimu hii ikawe chachu kwenu na ninyi mlio hapa mkawe mabalozi kwa wenzenu,huu siyo muda wa kutembea na kitita cha fedha mfukoni fungueni akaunti na mjiwekee desturi ya kuweka fedha benki ambako kuna mifumo salama ya kifedha,” ameongeza Nkinda.

Aidha, amewasisitiza kutumia mikopo wanayoipata kutoka taasisi za kifedha kwa tija kwa kuzingatia mipango na bajeti, pamoja na kuelekeza fedha hizo katika shughuli halali za maendeleo hasa ununuzi wa madini kwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.
“Jambo lingine muhimu ni matumizi yah ii mikopo ambayo tunachukua kwenye taasisi za kifedha,naomba mkaitumie kwa shughuli za kiuchumi na pesa zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa Pamoja na ununuzai wa dhahabu,asitokee mtu anakopa fedha anaenda kununua gari au kufanya sherehe,” amesisitiza Nkinda.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Benki ya Tanzania Tawi la Mwanza, Mukrim Ramadhani amesema mafunzo hayo yanahusu masuala ya usimamizi binafsi wa fedha, uwekezaji katika dhamana za serikali, ununuzi wa madini, pamoja na udhamini wa mikopo kutoka mabenki ya biashara.
Ameongeza kuwa washiriki pia wanaelimishwa juu ya umuhimu wa kutumia mifumo rasmi ya kifedha ili kudhibiti matumizi ya fedha taslimu, kupunguza hatari ya wizi, pamoja na namna ya kuifikia Benki Kuu wanapokuwa na malalamiko.

“Leo tupo katika mafunzo haya lengo ni kukumbushana na kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha ili kudhibiti matumizi ya fedha taslimu hali itakayosaidia kupunguza wizia upotevu wa fedha,” amesema Ramadhani.
Mmoja wa wachimbaji walioshiriki mafunzo hayo, Cosmas Maghati kutoka Mgodi wa Mwime, amesema wengi wao wamekuwa wakikosa elimu ya matumizi sahihi ya fedha hali inayowafanya kutokuwa na kumbukumbu nzuri za mapato na matumizi na kushindwa kuwekeza katika miradi ya kimkakati.

‘Tunashukuru sana kwa elimu hii kwani wengi wetu hatuna elimu ya matumizi sahihi ya fedha hali inayotufanya kutokuwa na kumbukumbu ya mapato na matumizi hali inayotufanya tushindwe kuwekeza miradi ya uchimbaji dhahabu kwa umakini,” amesema Maghati.