Na Saulo Stephen – Singida.
Ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi umefikia asilimia 101, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa katika kuimarisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussein Simba amesema, mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa vyanzo vya mapato na amewataka madiwani kuendelea kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao.

Akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Halmashauri, amesema ni muhimu kuhakikisha kila eneo linachangia katika kuongeza mapato na kufikia malengo yaliyowekwa.
Amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa vyanzo vya mapato, hatua itakayoiwezesha Halmashauri kuongeza mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema ongezeko la mapato litasaidia kuimarisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi wa Wilaya ya Itigi.


