Mawaziri wa Ulinzi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels wameshindwa kufikia makubaliano kuhusu kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za mataifa hayo kushambulia ndani ya ardhi ya Urusi.
Nchi hizo zilishapitisha makubaliano ya pamoja ya kuipatia msaada wa silaha nchi hiyo,hata hivyo baadhi ya nchi wanachama zimetoa silaha zao kwa masharti ya kuitaka Ukraine isizitumie kushambulia ndani ya ardhi ya Urusi.
Serikali ya mjini Kiev inasisitiza kwamba wanajeshi wake wanahitaji kuruhusiwa kushambulia ndani ya Urusi kwa sababu vikosi vya nchi hiyo vinashambulia kutoka ndani ya ardhi yake kwenye maeneo ya mipaka.
Rais Emmanuel Macron ambaye jana alikutana na Kansela Olaf Scholz karibu na mji wa Berlin aliunga mkono hatua ya kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za nchi za Magharibi kushambulia ngome za kijeshi za Urusi ndani ya nchi hiyo,wakati Scholz akijizuia kutowa msimamo kama huo,japo alisema Ukraine inayo haki ya kijilinda.