Na Gideone Gregory,Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema kwa upande wa wanawake walioolewa, vitendo vya unyanyasaji wa kimwili, kingono, au kihisia vimepungua kutoka 50% mwaka 2015/2016 hadi 39% mwaka 2022/23.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yaliyoambatana na uzinduzi wa mpango kazi wa taifa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto awamu ya pili (MTAKUWWA II) na kuongeza kuwa kiwango hicho kinapungua lakini bado ni kikubwa kwa wanawake na watoto.
Aidha Dkt. Gwajima ameongeza kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024, Wizara na Wadau kupitia Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Wazazi na Walezi Katika Malezi ya Watoto na Familia imeendelea kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii kupitia redio na runinga, mikutano na makongamano yanayohusisha wananchi na mitandao ya kijamii.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya ameiomba serikaki wanaobaka watoto chini ya miaka kumi wasidhaminiwe kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la watoto wadogo kubakwa.