Na Gideon Gregory – Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeazimia kuwa Serikali ihakikishe ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa unakamilika ifikapo Aprili, 2025 na iandae mkakati wa kuanzisha chombo maalum cha usimamizi wa Uwanja huo na viwanja vingine vinavyojengwa na Serikali, ili kuhakikisha vinatunzwa na kuwa katika ubora wa kimataifa.
Ushauri huo umetolewa leo Bungeni Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na michezo, Husna Juma Sekiboko wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/426eeaf9-4539-4b32-ba98-ac3ee3cbdb6f.jpg)
“Uwanja huo pamoja na viwanja vingine vya michezo unahitaji matengenezo ya mara kwa mara ili kudumisha ubora wake wa kimataifa na kuimarisha maendeleo ya sekta ya michezo nchini,” amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuweka utaratibu wa sehemu ya makusanyo ya uwanja kubaki kwa matumizi ya uwanja huo (Retention) ili kurahisisha matengenezo ya dharura yanapojitokeza.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Tanzania_National_Main_Stadium_Aerial-1024x597.jpg)
“Serikali iandae mkakati wa kuboresha viwanja vingine vya michezo ili kupunguza mzigo wa matumizi makubwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa,” amesema.
Sekiboko amebainisha kuwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa ni moja ya miundombinu muhimu ya michezo nchini inayotumiwa kwa matukio ya kitaifa na kimataifa, lakini unakabiliwa na changamoto za matengenezo na usimamizi endelevu.