Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kukarabati miundombinu ya Mnada wa Bitalanguro uliopo Bunda ambapo kwasasa wamekamilisha ujenzi wa choo, ofisi na uzio, hivyo wanaendelea kufanya ukarabati taratibu kadri fedha zinavyoendelea kupatikana.
Hayo yameelezwa leo Aprili 15,2025 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti wakatia akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Ester Bulaya kwa niaba ya Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere aliyehoji ni lini Serikali itahakikisha inaweka mazingira rafiki ya mradi wa Bitalaguro ili wafugaji waweze kwenda kuuza mifugo yao kwenye mnada wenye staha.
“Ni muhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara fedha zinapopatikana tutapeleka kwenda kukarababti, lakini pia niiombe Halmashauri kwasababu inapata mapato kutoka huko iweze kukarabati katika miundombinu midogo midogo ambayo ambayo inahusiana na maeneo yao,”amesema.
Awali akijibu swali la nyongeza la Mbunge Gutere juu ya lini Serikali itakamilisha ahadi ya ujenzi wa mnada wa Mifugo Mngeta – Bunda, Mnyeti amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali haikuweka kwenye mpango ujenzi wa minada mipya hapa nchini ili kutoa fursa ya ukamilishwaji wa minada 23 ya awali iliyopo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
“Serikali ina jukumu la moja kwa moja la kujenga na kuendesha minada ya upili na mpakani hivyo, Wizara itaendelea kuweka katika mpango wa bajeti ujenzi wa minada ya awali nchini ikiwemo mnada wa Mifugo Mngeta kulingana na upatikanaji wa fedha,” amesema.
Pia, ameongeza kuwa Katika bajeti ya Mwaka 2023/2024 Serikali ilitenga jumla ya shilingi 435,238,870 kwa ajili ya ujenzi wa mnada wa Bitalaguro uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
“Mwezi Februari, 2025 ujenzi wa mnada huo ulikamilika. Hivyo, kukamilika kwa ujenzi wa mnada wa Bitalaguro utatoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ya Bunda kuuza na kununua mifugo katika mnada huo,” amesema.