Na Daniel Gahu – Katavi.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amepokea makundi sita yenye jumla ya madaktari bingwa na ubingwa bobezi 30 pamoja na wauguzi bingwa watano watakaotoa huduma katika Hospitali za Wilaya na ya rufaa Mkoa wa Katavi kwa siku tano.
Akiwapokea Madaktari hao hii leo Septemba 29, 2025 katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, amesema ujio wao utakwenda kuwajenga Madaktari waliopo katika Hospitali za mkoani hapa na kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kutokana na uzoefu watakaoupata.

“Pamoja na kuwa wananchi wanaenda kunufaika na huduma za kibingwa kuwa karibu na maeneo yao lakini pia madaktari hawa wataenda kuacha ujuzi kwa madaktari wetu ambao utawawezesha kuongeza ufanisi wa huduma baada ya siku tano za kupata uzoefu kutoka kwa madaktari bingwa,” amesema Mrindoko.
Akizungumza wakati wa kuwatambulisha madaktari hao Mratibu wa program ya mama na mtoto kutoka wizara ya afya Luciano Lodrick, amesema madaktari watakwenda kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za halmashauri za wilaya ya Tanganyika, Nsimbo, Mlele, Mpimbwe na Manispaa ya Mpanda kwa siku tano.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt Jonathan Budenu amesema kwa sasa Mkoa huu unaongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kutokana na wananchi wengi kubadili mtindo wa maisha ikiwepo kutokuzingatia lishe bora.
Nao wananchi wa Mkoa wa Katavi, wameishukuru Serikali kwa kutambua uwepo wao na kuwasogezea huduma za kibingwa ndani ya maeneo yao ya karibu, hii ni kutokana na huduma za kibingwa kutokuwepo ndani ya Hospital zote za Mkoa, hivyo ujio wa madaktari bingwa utarahisisha upatikanaji wa huduma za kimatibabu ya kibingwa.

“Hakika ujuio wa Madaktari hawa watasaidia upande wa kuokoa gharama za safari kwenda mikoa jirani ya Mbeya, Tabora na Mwanza ambapo tulikuwa tunazifuata huduma za matibabu ya Kibingwa,” amesema Mzee Mkuyu.


