Na Gideon Gregory – Dodoma.
Serikali imesema ujenzi wa soko la mnada wa mifugo katika Jimbo la Meatu unatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2026 ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26 Halmashauri imetenga shilingi milioni 12 kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa uzio wa mnada katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mnada wa kisasa wakati taratibu za kutafuta fedha za ujenzi wa mnada huo zikiendelea.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 24,2026 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Meatu, Salum Khamis Salum aliyehoji ni lini serikali itaanza ujenzi wa soko la mnada wa mifugo ili kuwa na soko lenye hadhi na kuongeza mapato ya Halmashauri katika Jimbo la Meatu.

Aidha, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Meatu inayo minada ya awali minne (4) ya Bukundi, Itinje, Mwanhuzi na Tindabuligi ambayo inahitaji kuboreshwa ili kuweka mazingira mazuri ya kuuza na kununua mifugo katika wilaya hiyo.
“Kwa kutambua umuhimu huo, mwaka 2023/24 Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kupitia mapato ya ndani ilitoa Shilingi milioni 14.3 kwa ajili ya kuboresha minada hiyo kwa kujenga machinjio, choo na kutwaa eneo la kujenga mnada wa kisasa lenye ukubwa wa ekari nane katika Kijiji cha Bukundi,” amesema.

Katika swali la nyongeza la Mbunge huyo juu ya upelekaji wa mizani katika minada hiyo, Dkt. Dugange amesema kwa kushirikiana na Wizara husika Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha eneo hilo linakuwa na mizani.


