UJENZI MELI ZA MIZIGO BANDARI YA KAREMA MWAROBAINI KWA BIASHARA KIMATAIFA

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amefanya ziara katika Bandari ya Karema iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa meli nne unaoendelea katika bandari hiyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, RC Mrindoko amesema mradi huo ni fursa kubwa kwa Katavi na Tanzania kwa ujumla, kwani Bandari ya Karema inatarajiwa kuwa kitovu cha biashara na uchumi, ikirahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima kwenda katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, ni wakati sasa wa kuzalisha mazao ya kutosha kwa ajili ya masoko ya ndani na nje, kwa kuwa bandari hii itakuwa lango la kibiashara litakalotuunganisha na masoko makubwa zaidi,” amesema RC Mrindoko.

Amesisitiza wananchi kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi na kuepuka kuuza kiholela ili kuhakikisha wanawanufaika na miradi ya kimkakati kama huu.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Bandari ya Karema, Antony Poyo amesema mradi huo umefungua fursa za ajira na kipato kwa wakazi wa eneo hilo kupitia ajira za muda na ushiriki wa jamii katika ujenzi na huduma mbalimbali.

Serikali kwa upande wake inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mpanda hadi Karema na mpango wa kuunganisha reli ya SGR, hatua ambazo zitalifanya eneo hilo kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara kwa ufanisi zaidi.

Wananchi waliojitokeza katika ziara hiyo ya ukaguzi wa ujenzi wa Meli nne kubwa za mizigo wamesema ujenzi huo ni fursa kwao kwani kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa kibiashara baina ya Tanzania na nchi zote zinazotumia ziwa Tanganyika kufanya biashara mbalimbali, bila kusahau mazao na mifugo”, amesema Amani Mahela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *