UJENZI LAMI YA BWANJAI MISSENYI KUCHOCHEA SHUGHULI ZA KIUCHUMI

Na Cecilia Shiratu, Missenyi – Kagera.

Wananchi wa Kata ya Bwanjai, Wilayani Missenyi mkoani Kagera, wameeleza matumaini yao kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa moja, inayogharimu zaidi ya shilingi milioni 400, kutachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Wamesema, mradi huo unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Michael Mwango’nda, amesema ameridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo.

Katika hatua nyingine Wango’nda amesema mwendelezo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni ya wavulana katika Shule ya Sekondari Bwanjai.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilika kwa mradi huo ndani ya mwezi mmoja, akibainisha kuwa serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake hivyo wasimamizi wa mradi pamoja na wadau wengine kuongeza kasi ya ujenzi, ili kuhakikisha mabweni hayo yanakamilika kwa wakati na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wao, Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bwanjai wameelezea changamoto zinazowakabili kutokana na ukosefu wa Mabweni ya Wavulana, Wanafunzi hao wamekua wakipata adha ya kutembea umbali mrefu kufika Shuleni, hali ambayo imekuwa ikiathiri mazingira yao ya kujifunzia.

Hata hivyo, kukamilika kwa mabweni hayo kutawawezesha kupata mazingira bora na salama zaidi, hali itakayosaidia kuongeza umakini katika masomo na kuboresha kiwango cha ufaulu.

Mradi wa ujenzi wa mabweni hayo unakadiriwa kugharimu shilingi milioni 130, ambapo wananchi wamechangia shilingi milioni 28, huku serikali ikitoa shilingi milioni 102 kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kuishi na kujifunzia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *