Na Saulo Stephen – Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amewataka walimu Mkoani humo kusimamia nidhamu kwa Wanafunzi, ili kuwajenga kuwa kizazi bora hata pindi wanapomaliza masomo waende kuwa wazazi bora katika Familia zao.
RC Dendego amyasema hayo wakati akizungumza na Walimu wa Mkoa wa Singida kwenye hafla ya utoaji tuzo za wadau wa elimu kwa shule zilizofanya vizuri pamoja na walimu waliofanya vizuri kwenye masomo wanayofundisha katika mitihani ya taifa, hafla iliyofanyika katika shule ya msingi Samamba iliyopo wilayani Ikungi Mkoani humo.

Amesema walimu licha ya kufanya kazi nzuri katika ufundishaji,pia wana wajibu mkubwa wa kusimamia nidhamu kwa wanafunzi wao,hasa pale ambao panatokea wanafunzi kulegalega katika suala la nidhamu walimu wanapaswa kutumia viboko ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa imara katika nidhamu na kutengeneza kizazi bora cha baadae.
Aidha katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amemuagiza Afisa Elimu Mkoa wa Singida Mwalimu Makwasa Bulenga kusimamia ipasavyo suala la chakula kwa Wanafunzi shule.

Aidha, hiyo pamoja na kuangalia utaratibu wa wanafunzi kubeba chakula kutoka nyumbani kila asubuhi wanapokwenda shuleni ili kuwafanya wanafunzi wawe na hali nzuri ya uelewa wa masomo yao kutokana na kuwa na uhakika wa kula na kushiba pindi wawapo shuleni.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Elimu Mkoa wa Singida Makwasa Bulenga amsema katika kuhamasisha zaidi ufundishaji na kuinua elimu Mkoani humo tuzo za Wadau wa elimu zitakuwa zikitolewa kila mwaka mara baada ya matokeo ya mitihani ya kitaifa.


