UJENZI KITUO CHA PAMOJA CHA FORODHA KUIMARISHA MAPATO YA SERIKALI – DKT. NYANSAHO

Na Tryphone Odace, Buhigwe – Kigoma.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema ujenzi wa Kituo cha pamoja cha forodha kilichopo Manyovu, Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, utaimarisha upatikanaji wa mapato ya Serikali pamoja na kuendelea kudumisha usalama katika eneo hilo la mpakani.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya kimkakati mkoani Kigoma, Waziri Nyansaho amesema kituo hicho kitakapokamilika na kuanza kutumika, kitasaidia kurahisisha utoaji wa huduma za forodha na kuongeza ufanisi katika shughuli za mipakani.

Waziri Nyansaho aliwataka wakazi wa Manyovu na maeneo jirani kuhakikisha wanatunza miundombinu ya kituo hicho ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kutoa huduma zinazokusudiwa.

Aidha, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Buhigwe kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu matukio au mienendo yoyote inayoweza kuhatarisha usalama, hususan kutokana na wilaya hiyo kuwa eneo la mpakani.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pia amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo–Kasulu–Manyovu Lot 1, inayohusisha kipande cha Kasulu–Manyovu chenye urefu wa kilomita 58.7.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa wakati wa ziara hiyo, ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na kwa sasa ipo katika kipindi cha matazamio.

Mradi huo unatarajiwa kuendelea kuchangia katika kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika maeneo yanayounganisha Kasulu na Manyovu.

Ziara ya Waziri Nyansaho mkoani Kigoma inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye umuhimu wa kimkakati, huku ikisisitiza umuhimu wa usalama, miundombinu na ustawi wa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *