Serikali mkoani Shinyanga imesema kuwa itaangalia upya utaratibu wa kuhamisha walimu kutoka vijijini kwenda mijini ili kuzuia ongezeko la shule za vijijini kukosa walimu na kusababisha wanafunzi kufeli.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha katika kikao kazi cha kutathimini hali ya elimu mkoa Shinyanga kilichofanyika wilayani kahama kikijumuisha Halmashauri ya Msalala,Ushetu na Kahama manispaa.

“Inabidi tuangalie upya utoaji wa Uhamisho kwa walimu,walimu wakipangiwa shule za vijijini wanakuja kuomba uhamisho,sasa uhamisho utatolewa kwa sasababu maalumu tu mana walimu wengi wanajaa mjini vijijini hakuna walimu,” amesema Macha.
Katika hatua nyingine Macha ameagiza kufungwa kwa vituo visiyo halali vya masomo ya ziada (Tution) na kwamba masomo ya ziada yafundishwe kwenye majengo rasmi ya shule.

“Hapa Kahama vituo vya Tution ni vingi Sana,unakuta banda mchana darasa la tution usiku banda la video,Sasa kuna haja kuzuia tution hizi na badala yake tution ziwe kwenye majengo maalum ya shule,” ameongeza Mkuu wa Mkoa Macha.
Awali akisoma tathimini ya hali ya elimu Afisa Elimu wa mkoa wa Shinyanga Bakari Kasinyo amesema kuwa mambo mengi yanayokwamisha Elimu ni Upungufu wa miundo mbinu,wanafunzi kukosa chakula shuleni pamoja na utunzaji wa mazingira.

“Changamoto kubwa shule nyingi ni miundo mbinu mibovu,na wanafunzi wengi katika baadhi ya Shule hawapati chakula Mashuleni na Mazongira mengi hayana Miti,Hizi baadhi ya sababu shule nyingi kutofanya vizuri,” amesema Kasinyo.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Msalala, Iddy Cassim amewataka walimu kupendana na kuwa wamoja ili kuinua sekta muhimu ya elimu.

“Kingine niwaombe walimu Kupendana,Mwalimu mkuu akimuona mwalimu wa kawaida anafanya vizuri anamuwekea Kinyongo akihisi utendaji wake utapindua cheo chake,hivyo tupendandane tuwasaidie watoto kusoma,” amesema Iddy.
