Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amekutwa na kesi ya kujibu katika kesi ya uhaini inayomkabili na inayoendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam.
Mahakama Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kusikiliza hoja na ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili ikieleza kuwa, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na maudhui yaliyomo kwenye hati ya mashtaka, imejiridhisha kuwa kuna msingi wa kisheria wa mtuhumiwa kuendelea kujitetea.

Kwa hatua hiyo, Lissu anatarajiwa kuanza hatua ya utetezi huku akiwataja mashahidi 11 watakaotoa ushahidi kwa upande wake.
Mashahidi hao, ni pamoja Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa zamani Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wa zamani Kassim Majaliwa pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillus Wambura.


