Ugonjwa wa Polio Kusitisha Mapigao kwa Muda Gaza

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao cha dharura Agosti 29,2024 makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ili kujadili mapigano yanayoendelea Gaza na eneo linalokaliwa na Israeli la Ukingo wa Magharibi huku likiripotiwa kuridhiwa kwa sitisho la mapigano ili kutoa fursa ya chanjo dhidi ya polio.

Mwakilishi wa WHO huko Gaza, Rik Peeperkorn amewaambia waandishi wa wa habari mapema leo Alhamisi jijini New York, kwa njia ya video kutoka Gaza kuwa “tuna ahadi za awali za sitisho la mapigano katika maeneo mahsusi wakati wa awamu pili za kampeni ya chanjo Gaza.

Amethibitisha kuwa kampeni hiyo itaanza tarehe Mosi Septemba katika Ukanda wa Gaza ambapo wakati wa awamu hizo za chanjo, Wizara ya Afya ya Palestina, kwa ushirikiano na WHO, UNICEF na UNRWA pamoja na wadau watapatia kila mtoto matone mawili ya chanjo mOPV2 kwa watoto zaidi ya 640,000 wenye umri wa chini ya miaka 10.

Ametoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo kusitisha mashambulizi ili kuruhusu watoto na familia zao kufikia kwa usalama vituo vya afya, halikadhalika wahudumu wa afya wanaotembea kwa miguu na magari kutoa huduma hiyo ya chanjo kwa watoto wasioweza kufikia vituo vya afya.

Wakati huo huo kaimu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA Joyce Msuya akihutubia Baraza hilo amesema wahudumu wa kibinadamu wanafanya kazi bila kuchoka kudhibiti kuenea kwa polio kwenye ukanda wa Gaza uliozingirwa na jeshi la Israeli, wakati huu ambapo mgonjwa mmoja amethibitishwa wiki iliyopita ikiwa ni miaka 25 tangu ugonjwa huo utokomezwe eneo hilo.

Naibu Mkurugenzi wa WHO Dkt. Mike Ryan kupitia baraza hilo amewaambia mabalozi kwamba kampeni dhidi ya polio inahitajika ili kuleta mabadiliko dhahiri kwenye mchakato mzima wa kusambaza misaada Gaza, ambao unapaswa kufanyika kwa kiwango kikubwa, kwa kasi kubwa na bila kikwazo chochote.

Mkutano huu umefanyika  katika wakati ambao kumekuwa na ongezeko la ghasia zinazofanywa na walowezi wa kiyahudi dhidi ya Wapalestina huko Ukingo wa Magharibi, sambamba na shambulio dhidi ya timu ya watendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP huko Gaza, tukio ambalo limesababisha shirika hilo kusitisha Oparesheni zake kwenye eneo hilo hadi itakapojulishwa tena.

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA linaendelea kuratibu na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa harakati za kusambaza chanjo dhidi ya polio baada ya ugonjwa huo uliokuwa umetokomezwa Gaza, kuibuka tena.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *