Nchini Uganda Watoto watano wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa usiojulikana ambapo ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwezi Januari katika vijiji sita vya wilaya ya Bukomansimbi katikati mwa nchi hiyo.
Baadhi ya wazazi waliopoteza watoto wao wameviambia vyombo vya habari kwamba ingawa walikimbilia hospitalini mara tu watoto wao walipohisi vibaya, madaktari hawakuweza kuokoa maisha yao kwa vile walikuwa wamechelewa.
Viongozi katika eneo hilo wameitaka wizara ya afya ya nchi hiyo kuchunguza kile kilichowaua watoto wao huku wakilalamikia uzembe wa maafisa wa afya wa eneo hilo.
Ugonjwa huo wa ajabu una dalili za homa kali, kutapika, kupauka, kutoa mkojo wenye damu, na udhaifu wa jumla wa mwili, ambapo kwa mujibu wa afisa wa afya wa wilaya hiyo Daktari Alfred Kato, amedai kwamba kuna uwezekano ilikuwa ni malaria kali.