Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wamelalamikia hali mbaya ya barabara katika maeneo mbalimbali, huku wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), ili ziweze kupitika.
Akizungumzia changamoto hiyo, naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ndala, Zamda Shabani amesema hali ya barabara ni mbaya na kuisihi TARURA kwamba wanapopata fedha, waanze kukarabati barabara zilizo katika hali mbaya zaidi.

Naye diwani wa Viti Maalum, kutoka kata kata ya old Shinyanga Pica Chogelo, amesisitiza umuhimu wa kupewa kipaumbele barabara zinazohudumia taasisi muhimu za kijamii kama shule na zahanati,hata kama fedha ni chache.
Akipendekeza mikakati yay a kukabiliana na changamoto hiyo ya ubovu wa barabara Diwani wa kata ya Lubaga Rubeni Dotto,amependekeza halmashauri inunue mtambo wake wa kutengenezea barabara ili kupunguza utegemezi kwa TARURA.

Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko naye amekiri kuwa barabara ni mbaya, na kuwataka madiwani kuacha kulalamika sana, kwani chanzo cha kutokurabatiwa kwa barabara nyingi katika manispaa hiyo chanzo kinajulikana kuwa ni ufinyu wa bajeti.
Akitolea ufafanuzi kuhusiana na ubovu huo wa barabara katika maeneo mengi ndani ya halimashauri ya manispaa ya Shinyanga Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga,Mhandisi Kulwa Maige, amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 waliidhinishiwa sh. bilioni 2.9, huku bajeti ya matengenezo ya barabara ikiwa Sh. bilioni 1.4, lakini mpaka sasa wamepokea Sh. milioni 85.4 pekee.

“Ufinyu wa bajeti ndiyo kikwazo kikuu katika matengenezo ya barabara ukilinganisha na urefu wa mtandao wa barabara tulio nao, katika utatuzi wa tatizo hili tunaomba halmashauri iwe inatenga fedha kupitia mapato yake ya ndani ili kusaidia ukarabati wa barabara, badala ya kuitegemea TARURA pekee,” amesema Mhandisi Maige.