Uelewa wa Lishe  ni Changamoto Ndani ya Jamii

Na,Ibrahim Rojala

Utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 unabainisha kwamba asilimia 3 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 nchini wana ukondefu kulingana na kigezo cha uzito na urefu wao, aidha, asilimia 12 ya watoto walio na umri chini ya miaka 5 wana uzito pungufu.

Licha ya viwango vya udumavu kupungua kutoka asilimia 50 mwaka 1991-92 hadi kufikia asilimia 30(Asilimia 30 ya watoto walio na umri chini ya miaka 5 wana udumavu (wafupi kwa kulinganishana kigezo cha umri wao) na asilimia 9 ya watoto wana udumavu mkali hali inayoonesha bado tatizo lipo, na kwa kutambua umuhimu wa Lishe kwa Mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya Miaka mitano,kwa nyakati tofauti tumefanya mahojiano na baadhi ya wananchi katika kata ya Mwakitolyo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ili kufahamu wana uelewa gani kuhusiana na lishe na kwa namna moja au nyingine wameonesha kuwa na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa lishe kwa makundi hayo mawili ambayo ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito.

Joyce Lulengo Bushosha,mama wa mtoto mmoja na mkazi wa Mwakitolyo yeye anasema huwa anasikia kuhusiana na masuala ya lishe lakini haelewi na kueleza kwamba katika  kipindi cha ujauzito  wake aliwahi kutumia mboga za majani mara moja na kuomba waendelee kupatiwa elimu ya lishe akieleza kwamba angependa kufundishwa chakula sahihi kinachoweza kumlinda mtoto aliye tumboni wakati wa ujauzito ili kumlinda mtoto hali itakayomuwezesha kujifungua salama.

Abdulmalik Paulo ni mmoja kati ya wazazi waliowahi kupata madhara ya ukosefu wa lishe kwa mama mjamzito,anaeleza kwamba miaka mitano iliyopita aliwahi kupata mtoto aliyezaliwa akiwa na unyafuzi na kueleza kwamba tangu wakati huo alijifunza kuzingatia kumuandaa mwanamke mjamzito kwa kumpatia lishe na kuwashauri wanaume wengine kuongozana na wake zao katika vituo vya Afya katika kipindi cha ujauzito na kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusiana na Afya.

Aidha licha ya juhudi kubwa za serikali katika kuhakikisha huduma bora za Afya na elimu ya lishe vinapatikana kwa akinamama wajawazito bado kuna changamoto,Muuguzi anayehusika na kitengo cha Uzazi, na Kinga kwa Watoto katika zahanati ya Mwakitolyo Ruben Venance Chisi anasema kwamba kwa upande wa lishe na hata matumizi ya dawa muhimu zinazopaswa kutumika wakati wa ujauzito mwitikio bado uko chini kwani baadhi ya wanawake hutupa dawa hizo

“Unakuta umempa dawa,baada ya mwezi akirudi,unapomuuliza zile dawa ulimeza mwingine anakwambia nilimeza zilizobaki hizi,na wakati mwingine hapa hapa karibu na zahanati ukipita unakuta dawa zilizotupwa”Amesema Chisi

Afisa Afya Kata ya Mwakitolyo Bw.James Kurwa anaeleza kwamba hakuna kesi nyingi kwa kundi la watoto zinazoashiria changamoto ya ukosefu wa lishe ingawa amashawahi kupata visa vichachache kuhusiana na lishe na kueleza kwamba bado jamii haina uelewa wa kutosha kuhusiana na Lishe.

“Kuna changamoto,unajua kuna familia nyingi uelewa ni mdogo,kuna watu wanaamini kuwa ili upate lishe bora ni lazima uwe na kipato kikubwa lakini kumbe unaweza kuwa na pesa kidogo lakini ule mpangilio wa vyakula ukasaidia,ndio maana tumejikita katika kutoa Elimu”amesema Kurwa

Afisa Afya wa Kata ya Mwakitolyo Bw.James Kurwa akiwa Ofisini kwake baada ya kukamilisha mahojiano na Mwandishi wa makala hii.

Aidha amesema miongoni mwa changamoto zinazoathiri upatikanaji wa lishe bora ni uwepo wa ugumu wa upatikanaji wa mboga za majani katika kata hiyo jambo aliloeleza kuwa linaweza kutumika kama fursa ya kiuchumi kwa watu kuwekeza katika kilimo cha mbogamboga na matunda na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya lishe bora kwa makundi yote ndani ya jamii.

“Mtu anaweza kuingia hotelini na kwa wakati mmoja anaweza kuagiza ugali,samaki na maharage bila kujua kinachopatikana katika maharage ndicho anachokipata kwenye samaki,angepata ugali, samaki na mchicha kidogo na kipande cha chungwa tungesema amebalance,hivyo hivyo hata majumbani unakuta mtu ana kuku lakini anashindwa hata kuchinja,ana ardhi mbolea itokanayo na mifugo aliyonayo lakini anashindwa kulima hata bustani ndogo”

Miongoni mwa matokeo ya ukosefu wa lishe bora ni pamoja na udumavu ambao huashiria hali ya lishe pungufu kwa muda mrefu na matokeo ya utafiti wa viashiria vya malaria kwa mwaka 2022 yanaeleza kuwa hali ya udumavu hupungua endapo elimu ya mama na hali ya uchumi wa kaya vitaongezeka na hili ni muhimu ili kuendelea kupunguza udumavu ambao hapa nchini vijijini upo kwa asilimia 33 na mijini ukiwa asilimia 21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *