Na,Ibrahim Rojala
Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh.Omari Kipanga amesema serikali imeendelea kuimarisha Elimu ya Watu Wazima kupitia Programu mbalimbali zilizo chini ya sekta ndogo ya elimu ya watu wazima na elimu ya nje ya mfumo rasmi na kubainisha kwamba kulingana na taarifa ya tathmini (ESA) ya mwaka 2024 katika programu ya mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu wazima na jamii kumekuwa na mwitikio chanya.
Mh.Kipanga amebainisha hayo hii leo bungeni jijini Dododma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mh. Shally Raymond aliyetaka kufahamu idadi ya vituo vinavyotoa elimu ya watu wazima nchini pamoja na idadi ya wanufaika wa elimu hiyo kwa ujumla.
“Jumla ya wanakisomo 97,217 wamenufaika katika vituo 1851 ambapo wanaume ni 39,789 na wanawake 57,428, kupitia mpango wa programu ya elimu ya msingi kwa walioikosa yaani MEMKWA kwa mwaka 2023 jumla ya wanafunzi 57,843 walinufaika katika vituo 5,257 wavulana wakiwa 32,141 na wasichana 25,702, katika mpango wa elimu changamani baada Elimu ya Msingi yaani Integrated Post Primary Education jumla ya wanafunzi 9,368 wamenufaika katika vituo 89 ambapo wanaume ni 5,036 na wanawake ni 4,332”Amesema Mh Kipanga
Aidha ameongeza kuwa kupitia programu ya Mpango wa Elimu changamani kwa vijana walio nje ya mfumo wa shule jumla ya vijana 42,183 wamenufaika na mpango huo kwa kutumia vituo 85 kati yao wavulana wakiwa 20,195 wasichana 21,988 na kwa upande wa elimu ya sekondari inayotolewa kwa njia mbadala wanafunzi wapatao 11,721 kati yao wavulana wakiwa 5,529 na wasichana 6,192 walidahiliwa kwa mwaka wa masomo wa 2023 na kujiunga na elimu hiyo katika vituo 777 kati ya hivyo vya serikikali vikiwa 160 na vinanavyomilikiwa na wadau binafsi 617.
“Katika matokeo ya Sensa ya watu na makazi eneo hili vile vile limeangaliwa la kujua kusoma,kuandika na kuhesabu,katika taarifa ya sensa 2022 inaonesha kwamba sasa hivi katika nchi yetu asilimia 17 ya Watanzania hawajui kusoma,kuandika wala kuhesabu,asilimia hii imeshuka kutoka asilimia 22 ya mwaka 2012,kwahiyo imeshuka kidogo lakini bado tunasema asilimia hii ipo kubwa kulingana na maisha ya sasa hivi na karne ya sasa hivi”ameeleza Mh. Kipanga
Ili kupunguza kundi la Watanzania wasiojua kusoma na kuandika Naibu Waziri Kipanga ameeleza kwamba Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala yaliyofanywa mwaka 2023 imeanzisha Idara pamoja na vitengo katika Halmashauri zote nchini vya Elimu ya watu wazima ngazi ya Msingi na Sekondari na kuteua Maafisa Elimu ya Watu Wazima kwa ngazi zote mbili pamoja na uwepo wa utekelezaji wa Programu changamani inayohusisha stadi za ujasiriamali na maisha ,mapishi na masuala ya uhifadhi wa mazingira .