UCHUNGUZI WAANZA AJALI YA BULLDOZER ILIYOJERUHI WANNE GEITA

Na Frank Aman – Geita.

Jeshi la Polisi Mkoani Geita, linafanya uchunguzi wa tukio la ajali husisha Bulldozer lenye Na. BGC-BD-002 mali ya Mgodi wa Backreef uliopo wilayani Geita lililosababisha majeruhi wanne na uharibifu wa nyumba tatu na nguzo ya moja ya umeme.

Tukio hili limetokea April 03, 2025 saa 2 usiku katika Kitongoji cha Isangilo, Kata ya Lwamgasa wilaya ya Geita.

Waliojeruhiwa ni Pauline Charles (35) na mtoto Majaliwa Charles (umri wiki mbili) wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya wilaya ya Geita. Wengine ni Philipo Ngh’abi (14) na Mussa Michael (09) walipata michubuko walitibiwa na kuruhusiwa.

Inadaiwa kwamba, siku hiyo Ramadhan Samson, Operator (dereva wa mtambo) akiwa kazini na mtambo huo alibainika kuiba mafuta kutoka kwenye tenki la mtambo huo kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine na kati yao wawili wamekamatwa (majina yanahifadhiwa); baada ya walinzi kubaini tukio hilo walianza kufuatilia ili wawakamate.

Ramadhani Samson alipogundua walinzi wanaelekea ilipo mashine, alikurupuka na kukimbia huku akiacha mtambo huo ulikuwa umewashwa ukajiongoza wenyewe na kwenda kugonga nyumba hizo na kuwajeruhi watu hao waliokuwa ndani kisha mtambo huo kukwama kwenye majaruba.

Uchunguzi wa tukio hili unaendelea kufanyika sambamba na kumtafuta  operator kwa ajili ya hatua za kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *