UCHAGUZI MKUU: HAMASA YA KUDUMISHA AMANI YAZIDI KUSHIKA KASI

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Zikiwa zimesalia takribani siku 11 kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, hamasa ya kudumisha umoja na utulivu imezidi kushika kasi nchini, Jijini Dodoma, mamia ya wananchi kutoka makundi mbalimbali ikiwemo vijana, viongozi wa dini, wafanyabiashara na watumishi wa umma wamejitokeza kwa wingi kuonyesha mshikamano wao kupitia matembezi ya amani.

Matembezi hayo yaliyoratibiwa leo Oktoba 18,2025 yalikuwa na lengo la kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda amani kabla, yamefanyika asubuhi ya leo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuzuia vurugu na misuguano ya kisiasa.

Akizungumza mara baada ya matembezi hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuilinda amani ya nchi bila kuruhusu migawanyiko.

 “Amani hii tumeirithi kwa gharama kubwa, hatupaswi kuichezea,lazima tuiheshimu na kuilinda kwa uchungu,” amesema kwa msisitizo.

Amefafanua kuwa Tanzania imejipambanua kama kisiwa cha amani barani Afrika, tofauti na mataifa mengi yanayokabiliwa na migogoro. 

Hata hivyo, amewaonya wananchi kuwa amani hiyo inaweza kupotea endapo haitalindwa.

 “Amani hupotea isipolindwa,ukosefu wa amani hujenga chuki, huondoa mapatano, hupoteza haki na kuchelewesha maendeleo ya watu,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Machifu wenzake Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Dodoma, Chifu Bilingi Yassir Ally wa Nne, amesema utulivu na mshikamano ni urithi ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni wajibu wa kila Mtanzania kuuenzi kwa vitendo.

“Amani ndiyo nguzo ya maendeleo, na sisi kama Machifu tuna wajibu wa kuhakikisha hakuna anayeichezea tunu hii,Ole wao watakaothubutu kuleta vurugu au kujaribu kuivuruga Dodoma, maana tutasimama imara kuilinda nchi yetu,” amesema Chifu Bilingi kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa ni haki ya kila raia kupiga kura kwa utulivu, akieleza kuwa kushiriki uchaguzi kwa amani ni heshima kwa Taifa na uthibitisho wa ustaarabu wa kisiasa wa Watanzania.

 “Si dhambi kumuombea kura Chifu mwenzangu Hangaya anayeonyesha maono ya kuendeleza amani,tunachotaka ni nchi iendelee kuwa tulivu na yenye upendo,” ameongeza Chifu huyo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Chacha Marwa ameeleza kuwa vijana wameamua kuunga mkono juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu wanaamini amani ndiyo msingi wa maendeleo na maisha bora.

 “Ukiheshimu kura, unalinda sauti yako,Ukilinda amani, unalinda maisha yako,kamwe tusitumie mikono yetu kuharibu amani,” amesema Chacha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wafanyabiashara Wadogo mkoa wa Dodoma (Machinga), Hawa Maulidi Athumani, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuienzi amani na kudumisha upendo, akibainisha kuwa biashara ndogo ndogo hukua katika mazingira tulivu pekee.

 “Biashara zetu hufanikiwa pale ambapo kuna utulivu,ni jukumu letu sote kulinda hali hii ili mambo yetu yaende kwa usalama,” amesema.

Amesema wao kama wafanyabiashara wanawajibika pia kama walezi wa jamii wana jukumu kubwa la kuhubiri amani majumbani, makazini na katika mikusanyiko yote.

 “Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuwa balozi wa amani,tukihifadhi amani, tunahifadhi vizazi vyetu,” amesema Madidi.

Dodoma imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani na utulivu, huku viongozi wa Serikali, jamii na makundi mbalimbali wakiapa kushirikiana kuhakikisha uchaguzi wa Oktoba 29 unakuwa wa amani, huru na wa haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *