UCHAGUZI MKUU: ACT-WAZALENDO WAENDELEZA MCHAKATO KUWAPATA WAGOMBEA

Na Clavery Christian – Kagera.

Chama cha ACT-Wazalendo kimeendelea na mchakato wake wa ndani wa kuwapata wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo hadi sasa watia nia 15 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge katika majimbo tisa ya Mkoa wa Kagera.

Mbali na watia nia hao wa ubunge, pia amejitokeza mtia nia mmoja wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amechukua fomu akiomba ridhaa ya chama chake kumpitisha kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoani Kagera, Evodius Justinian amesema zaidi ya asilimia 75 ya watia nia kwa nafasi mbalimbali wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho, huku mwisho wa kuchukua fomu ukitarajiwa kuwa Julai 30, 2025.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama chake ya kugombea Urais, Aron Kamugisha Kalikawe alisema kipaumbele chake kikuu ni kuondoa umasikini nchini Tanzania, kutoa ajira kwa vijana, na kuhakikisha kila Mtanzania analipwa mshahara wa angalau shilingi 150,000 kwa mwezi.

“Nia yangu ni kujenga taifa la haki, fursa na ustawi kwa wote. Vijana watapatiwa ajira, na kila Mtanzania atapata mshahara wa kuishi kwa heshima,” alisisitiza.

Aidha Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Kagera Mchakato wa kuchukua fomu unaendelea nchi nzima, huku chama hicho kikisisitiza uwazi, usawa na ushindani wa haki miongoni mwa wanachama wote wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali kupitia ACT-Wazalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *