UBUNIFU UJENZI DARAJA LA MAWE MISUNGWI WAIPAISHA TARURA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kwa ubunifu wa kujenga daraja kwa kutumia mawe.

Ubunifu huo, umetajwa kuwa na tija kwa Taifa kwani unapunguza gharama za ujenzi wa miundombinu na kuokoa fedha zitumikazo kwenye miradi mingine, hususan vijijini ambavyo bado havifikiki vizuri.

Akizindua daraja hilo Agosti 16, 2026, katika Barabara ya Ngudama-Kaluluma linalowaunganisha wakazi wa Kata za Bulemeji na Idetemya Wilaya ya Misungwi, Mwang’onda amesema limegharimu Shilingi Milioni 122.59 na ulitekelezwa na mkandarasi M/s Bareez Investment Ltd.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi amesema, awali Wananchi wa Bulemeji na Idetemya walikumbana na adha ya barabara mbovu ambayo iliwalazimu kutumia muda mrefu na gharama kubwa kusafirisha mazao kwenda masokoni.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kushirikiana na TARURA kuondoa changamoto hiyo ambayo ilikuwa kikwazo kwa shughuli za kiuchumi.

Shughuli zilizofanyika katika ujenzi wa daraja hilo ni pamoja na kujenga boxi kalavati, kujaza mawe, kuweka zege la usafi, kujenga msingi wenye nondo, kuta za mawe na kingo, pamoja na kuweka alama za barabarani. TARURA imesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza usalama na uimara wa daraja hilo kwa manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *